Rais wa klabu bingwa nchini Hispania Real Madrid Florentino Perez, amesema hatojiingiza kwenye dili la kumsajili mshambuliaji kutoka England na klabu ya Tottenham Hotspurs Harry Kane.

Perez amefafanua suala la kujiweka pembeni katika biashara hiyo kwa kusema endapo wataingia kwenye harakati za kumsajili mshambuliaji huyo, Spurs watatangaza dau kubwa la pesa ambalo litamfanya Kane kuwa mchezaji ghali duniani.

Perez ameiambia radio Cadena Cope kuwa, kwa sasa mshambuliaji Neymar ndio anashikilia rekodi ya kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha pesa (Euro milioni 200.6), hivyo anaamini kwa Kane itakua zaidi ya hapo.

“Suala la kumsajili Harry Kane bado halijapitishwa kichwani mwangu,” alisema Perez. “Kweli ni mchezaji mzuri na bado kijana, lakini sina mpango wa kujiingiza kwenye usajili wake.

“Ana muda mrefu sana wa kucheza soka lake, na itapendeza kuwa na mazingira mapya katika maisha yake ya soka, lakini kwa sasa ninaridhishwa na kikosi tulichonacho, na sioni sababu ya kuamua kuingia gharama zaidi.”

Real Madrid wamewahi kuhusishwa na mpango wa kutaka kumsajili Kane mwenye umri wa miaka 24, huku meneja Zinedine Zidane akitajwa kuwa chanzo cha harakati hizo, itakapofika mwezi januari mwaka 2018.

Mara kadhaa Zidane amekua akimpongeza Kane kwa kazi nzuri anayoifanya akiwa na Sprus pamoja na timu ya taifa lake la England, hali ambayo inaendelea kudhihirisha namna anavyohitaji kuwa nae karibu.

Rosa Ree aachana na ‘The Industry’
Zitto kabwe asema yuko tayari kuwajibika