Klabu ya Newcastle Utd, ina matumaini makubwa ya kumsajili beki kutoka nchini Ufaransa na klabu ya Eibar ya Hispania Florian Lejeune, wakati wowote ndani ya juma hili.
The Magpies wanaendelea kufanya mazungumzo na uongozi wa Eiber na wamethibitisha kuwa katika hatua za mwisho za uhamisho wa beki huyo, mwenye umri wa miaka 26 ambaye atawagharimu kiasi cha Pauni milioni 8.7.
Endapo Lejeune atasajiliwa na Newcastle Utd, itakua ni mara yake ya pili kucheza soka nchini England, baada ya kufanya hivyo akiwa na Man city msimu wa 2015/16, lakini msimu uliofuata alipelekwa kwa mkopo kwenye klabu inayoshiriki ligi daraja la pili nchini Hispania Girona.
Klabu nyingine zilizowahi kupata huduma ya mchezaji huyo ni Auxerre ya nchini kwao Ufaransa, pamoja na Villarreal ya Hispania.
Eibar ilimsajili Lejeune kwa ada ya uhamisho ya pauni milioni 1.2, na msimu uliopita alicheza michezo 34 na kutoa mchango wa kuiwezesha klabu hiyo kumaliza katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi ya Hispania (La Liga).
Katika hatua nyingine Newcastle Utd wameendelea kuwa na matumaini makubwa ya kumnasa kwa mkopo mshambuliaji wa mabingwa wa soka nchini England (Chelsea) Tammy Abraham, ambaye kwa sasa anaitumikia timu ya taifa ya nchi hiyo chini ya miaka 21 kwenye michuano ya vijana ya UEFA inayoendelea nchini Poland.
Hata hivyo katika mpango huo Newcastle Utd huenda wakapata upinzani mkali kutoka kwa Brighton na Swansea, ambao wameonyesha nia ya kumsajili Abraham kwa mkopo.