Klabu ya Fluminense imeipiga chini ofa ya Majogoo wa jiji ‘Liverpool’ inayomlenga Kiungo kutoka Brazil André Trindade da Costa Neto, yenye thamani ya Euro Milioni 30.

Klabu hiyo ya Merseyside inamtaka André ajiunge nao kabla ya dirisha la usajili kufungwa Septemba Mosi, lakini Fluminense wanasita kumruhusu mchezaji huyo wa kimataifa wa Brazil kuondoka kabla ya mwisho wa msimu wao.

Bodi ya Fluminense iliifahamisha Liverpool hata kama wangetoa ofa kwa André hawatamruhusu mchezaji huyo kuondoka kwa sasa.

Liverpool wanahitaji kuimarisha safu yao ya kiungo kufuatia kuondoka kwa Fabinho na Jordan Henderson waliokwenda Saudi Arabia.

Fabinho alijiunga na Al Ittihad kwa uhamisho wa euro milioni 40 tangu Julai 31, mwaka huu huku Henderson akihamia Al Ettifaq kwa dili la euro milioni 14.

Chini ya mkataba na Fluminense hadi Desemba, mwaka 2026, Andre mwenye umri wa miaka 22 ni mchezaji muhimu wa Kocha, Fernando Diniz.

Amecheza mechi 40 za timu hiyo msimu uliopita na amevutia hisia za klabu kadhaa za Ulaya. Fulham walikuwa na ofa ya euro milioni 20 kwa André iliyokataliwa mapema mwaka huu.

Fluminense wana matumaini makubwa ya kushinda Copa Libertadores (Ligi ya Mabingwa Amerika Kusin) msimu huu.

Zimbabwe: Wakamatwa kwa kujumlisha matokeo
Msuva kutambulishwa rasmi JS Kabyile