Klabu ya Arsenal huenda ikapata ahueni kidogo kwenye mkwanja kunasa huduma ya kiungo Declan Rice kwa kuwa kuna kiasi kitarudi kutokana na West Ham United kuhitaji saini ya Mshambuliaji Folarin Balogun.
Arsenal ipo kwenye hatua za mwisho kutoa Pauni 105 milioni kunasa saini ya Kiungo na Nahodha wa West Ham ukiwa ni mpango wa kuboresha kikosi kwenye dirisha hili la uhamisho wa majira ya kiangazi.
West Ham imegoma kupunguza bei ya Rice, huku ikitaka mkwanja wote ulipwe ndani ya miezi 18, wakati Arsenal ilitaka ilipe miaka mitano.
Hilo lishamalizwa, lakini kocha wa West Ham, David Moyes anapanga kutumia pesa hizo kurudi Arsenal kumchukua Balogun.
Mshambulaiji huyo mwenye umri wa miaka 22 alionyesha kiwango bora alipokuwa kwa mkopo Reims ya Ufaransa alikofunga mabao 22 katika mechi 39.
Balogun anataka kuachana na Arsenal ikiwa ni mchakato wa kutafuta timu itakayompa nafasi ya kucheza kila mechi na West Ham inaweza kunasa saini ya mkali huyo wa Marekani.
Kwenye mauzo ya Mshambuliaji huyo, Arsenal inahitaji kati ya Pauni 30 milioni na Pauni 50 milioni, hivyo kama West Ham watamchukua kwa Pauni 50 milioni, hiyo itakuwa nafuu kwa Arsenal na kuonekana kama wamepata punguzo la bei kwenye usajili wa Rice kutoka West Ham, ambao wanahitaji Mshambuliaji mpya.
West Ham wanataka kutumia pesa za Rice kumsajili Harvey Barnes na James Ward-Prowse.