Kiungo mchakarikaji (Mkata Umeme) wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara (VPL) na Kombe la Shirikisho (ASFC) Simba SC, Gerson Fraga, amewashtua mashabiki wa klabu hiyo baada ya kuondoka nchini ghafla na kurejea kwao Brazil.

Fraga ameondoka klabuni hapo, wakati kikosi cha mabingwa hao kikitarajiwa kushuka Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Jumapili kuivaa Namungo FC kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mbelgiji Sven Vandenbroeck, amethibitisha kuondoka kwa kiungo huyo, ambapo amesema amelazimika kuondoka baada ya kupewa taarifa anatakiwa nyumbani kwa sababu ya matatizo ya kifamilia.

Amesema atalazimika kumkosa nyota huyo kwa muda mfupi kabla ya kurejea nchini kuendelea na majukumu yake, kwa sababu ni miongoni mwa wachezaji walikuwapo katika programu zake kwa msimu mpya wa 2020/21.

“Fraga amepata ruhusa maalum na ameenda kwao kuweka sawa matatizo ya familia yake, baada ya kumaliza atarejea mapema na kuungana na wenzake katika kuendelea na majukumu yake ya kazi,” amesema Sven.

Amesema anatarajia ndani ya wiki hii kikosi chake kitakamilika baada ya beki Pascal Wawa kutua nchini hii leo akitokea nchini kwao baada ya ruhusa maalum.

Kwa upande wa Fraga, amewaondoa hofu mashabiki wa Simba kwa kusema ameondoka kwa ajili ya matatizo ya kifamilia pekee, na atatejea mapema kuendelea na majukumu yake ya kazi.

“Mashabiki wanatakiwa kupotezea mitandao ya kijamii hasa kuhusu barua ambayo ilikuwa ikisambaa, mimi bado nipo Simba kwa mujibu wa mkataba wangu,” amesema Fraga.

Nyota huyo alikuwapo katika tamasha la Simba Day, na alicheza kipindi cha pili kama beki wa kati wakati wakishinda mabao sita kwa sifuri Uwanja wa Mkapa dhidi ya Vital’O ya Burundi.

Zahera: Wanaombeza Yondani hawajui mpira
Idara za serikali chapeni kazi zenu TSN