Klabu ya Villarreal inayoshiriki ligi kuu ya soka nchini Hispania, imemfuta kazi kocha Fran Escriba, kufuatia mwenedo wa kikosi cha klabu hiyo kuwa mbaya tangu walipoanza msimu wa 2017/18.

Jana kikosi cha Villareal kilikubali kupoteza mchezo dhidi ya Getafe kwa kufungwa mabao manne kwa sifuri, hali ambayo imeongezea makali kwa viongozi kumfuta kazi kocha huyo.

Mbali na mchezo wa jana, pia Villareal wamepoteza michezo mingine ya ligi ya Hispania chini ya utawala wa Escriba dhidi ya Levante na Real Sociedad, huku wakitoka sare na Espanyol.

Mpaka sasa Villareal wamefanikisha kushinda michezo miwili dhidi ya Real Betis na Alaves, hali ambayo inaifanya klabu hiyo kushika nafasi ya 14 kwenye msimamo wa ligi ya nchini Hispania (La liga).

“Villarreal imeamua kusitisha mkataba na Fran Escriba,” imeeleza taarifa ilitotolewa huko El Madriga. “Saa kadhaa zijazo, uongozi wa klabu utatangaza jina la kocha mpya, ambaye atakiongoza kikosi cha Villareal katika michezo inayofuata.”

Escriba alitangazwa kuwa kocha mkuu wa Villareal Agosti 2016 na mwezi Mei mwaka huu alisaini mkataba mpya ambao ulitarajiwa kufikia kikomo mwishoni mwa msimu huu.

Villarreal walipanda daraja na kucheza La Liga mwaka 1998, na miaka 10 baadae walifanikiwa kumaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Real Madrid.

Klabu hiyo maarufu kwa jina la Nyambizi ya Manjano (Yellow Submarine), ilishuka daraja mwaka 2012, lakini msimu mmoja baadae ilirejea ligi kuu na kucheza michuano ya Europa League.

Sakata la Neymar na Cavani lachukua sura mpya
Mwakyembe apiga marufuku tuzo za muziki na mashindano ya Miss Tanzania