Aliyekuwa Kocha Mkuu wa Biashara United na Kagera Sugar, Francis Baraza anatajwa kuwa miongoni mwa makocha wanaowindwa na Geita Gold FC kurithi mikoba ya Fred Felix ‘Minziro’ ambaye aliachana na klabu hiyo, lakini mambo yamegonga mwamba baada ya Polisi Kenya kutibua mambo.

Tayari Geita Gold FC ilikuwa imeshamalizana na Baraza kwa makubaliano ya mkataba wa mwaka mmoja na alikuwa anasubiriwa kuja nchini kusaini dili, lakini baada ya klabu yake ya Polisi Kenya kupata taarifa hizo fasta ikamuita chemba na kumuongezea mkataba.

Baraza ambaye aliisaidia Polisi kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Kenya, amesema kuwa kipaumbele chake kilikuwa kurudi Bongo msimu ujao ila ofa iliyowekwa mezani na waajiri wake imemshawishi kubaki Kenya.

“Kwa kweli nilikuwa nishapanga kurudi Bongo, lakini mabosi wangu wa Kenya Polisi walipata hizo tetesi na kufikia jana tulikuwa na mazungumzo baina yangu na viongozi. Kweli tumeweza kuafikiana na kuniongezea mkataba mwingine wa mwaka mmoja tena.

“Wamefanya hivyo kwa kuwa nimeifikisha timu katika nafasi ya tatu ligi yetu. Geita Gold ndiyo timu niliyokuwa nimeshakubaliana nao mkataba wa mwaka mmoja ila ndiyo hivyo bwana,” amesema Baraza.

Akizungumzia mchakato wa kocha mpya, Ofisa Habari wa Geita Gold, Hemed Kivuyo amesema uchujaji wa makocha kumpata mrithi wa Minziro haujaanza.

“Bado uongozi haujaanza kuchuja makocha na mpaka sasa hakuna makocha wa kigeni walioomba,” amesema.

Bangala, Djuma Shaban wabanwa Young Africans
Pep Guardiola akutana na Declan Rice