Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin amesema siku saba za maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa mwisho wa ‘Kundi D’ dhidi ya USGN ya Niger zinatosha kusuka mipango ya kuibuka na alama tatu.

Simba SC itaikaribisha USGN ya Niger Uwanja wa Benjamin Mkapa Jumapili (April 03) kuanzia saa moja usiku, huku ikitakiwa kushinda ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Robo Fainali.

Kocha Pablo amesema kikosi chake kitaingia kambi baada ya Michezo ya Kimataifa ya Kirafiki kwa mujibu wa kalenda ya FIFA, kuanza maandalizi rasmi ya kuikabili USGN.

“Baada ya kurejea kambini tutakuwa na wiki moja hivi ya kufanya maandalizi naimani inatutosha kwetu kwa kila mchezaji kufanya kile kinacho hitajika na kufanya vizuri katika mchezo wa USGN.”

“Malengo makubwa ni kufuzu katika hatua inayofuata kutokana na kiu ya mafanikio tuliyokuwa nayo naimani kubwa hilo linawezekana ingawa tutakuwa na mchezo mgumu kutokana na wapinzani wetu nao wananafasi kama ya kwetu.” amesema Kocha Pablo

Tayari Simba SC imeshaanza kuuza tiketi za mchezo huo utakaopigwa saa moja usiku, huku Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ likitoa kibali cha mashabiki 35,000 wataoshuhudia mchezo huo wakiwa Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kabla ya mchezo huo wa mwisho, Msimamo wa ‘Kundi D’ unaonyesha ASEC Mimosas inaongoza ikiwa na alama 09, ikifuatiwa na RS Berkane yenye alama 07 sawa na Simba SC huku USGN ikishika nafasi ya nne ikiwa na alama 05.

Cedric Kaze awachambua Farid Mussa, Bangala
Sakho afichua siri za vikao Simba SC