Homa ya Pambano la Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Young Africans imemkamata Kocha Mkuu wa Simba SC Franco Pablo Martin, baada ya kukiri ana kazi kubwa ya kufanya.
Pambano hilo limepangwa kuunguma Jumamosi (Mei 28), Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, huku timu hizo zikitarajiwa kukutana kwa mara ya nne msimu huu 201/22.
Tayari Miamba hiyo ya Soka la Bongo imeshakutana mara mbili kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na kuambulia sare ya 0-0, huku Young Africans ikichomoza na ushindi wa 1-0 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii mwanzoni mwa msimu huu.
Kocha Pablo amesema kuna tatizo kubwa kwenye kikosi chake, baada ya kucheza michezo miwili dhidi ya Azam FC na Geita Gold FC bila kupata ushindi, na hii imetokana na kutokuwajibika ipasavyo kwa wachezaji.
Amesema timu yake yote haikucheza vizuri kwenye michezo hiyo miwili ya Ligi Kuu waliyocheza ugenini, hivyo Benchi la Ufundi la Simba SC, lina kazi ya kufanya kuelekea mchezo dhidi ya Young Africans Jumamosi.
“Kwa sasa timu nzima inacheza vibaya kuanzia nyuma mpaka eneo la Ushambuliaji, pia tuna Majeruhi wengi, Kapombe, Inonga, na Bocco ameongezeka kwenye list ya Wagonjwa.”
“Kwa sasa Tumevunjika moyo, kimwili, kiakili na hiki ndio Kiwango chetu kuelekea Jumamosi dhidi ya Young Africans.” amesema Kocha Pablo
Simba SC ilitinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ kwa kuifunga Pamba FC mabao 4-0, huku Young Africans ikiibanjua Geita Gold FC kwa changamoto ya mikwaju ya Penati, baada ya sare ya 1-1 ndani ya dakika 90.