Meneja wa klabu ya Crystal Palace Frank de Boer amezima mipango ya mshambuliaji wake kutoka nchini Ubelgiji Christian Benteke, kuondoka klabuni hapo katika kipindi hiki cha majira ya kiangazi.
De Boer amezima fununu hizo akiwa katika matayarisho ya kikosi chake huko mashariki ya mbali (Hong Kong), ambapo amewaambia waandishi wa habari kuwa, hana mpango wa kumuachia mshambuliaji huyo.
Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi amesema Benteke ni mshambuliaji wa kipekee, na ana matarajio makubwa ya kuisaidia Crystal Palace katika msimu mpya wa ligi ya England ambayo itaanza mwezi ujao.
Benteke alikua ameanza kuhusishwa na mipango ya kusajiliwa na klabu ya Everton kama mbadala wa mshambuliaji Romelu Lukaku aliyeondoka Goodison Park na kutimkia Man Utd juma lililopita.
Klabu ya Chelsea nayo imewahi kutajwa kwenye harakati za kutaka kumsajili mshambuliaji huyo kwa lengo la kuiongezea makali safu yake ya ushambuliaji.
Benteke aliiongoza vyema safu ya ushambuliaji wa Crystal Palace msimu uliopita na kufanikiwa kufunga mabao 15 katika michuano yote aliyocheza, hali ambayo imeendelea kumuongezea uaminifu kwa Fank De Boer, ambaye amechukua nafasi ya Sam Allardyce huko Selhurst Park.