Meneja mpya wa klabu ya Inter Milan Frank de Boer, ameainisha mipango yake maalum ambayo itasaidia kuirejeshea heshima klabu hiyo ya mjini Milan kama ilivyokua miaka iliyopita.

De Boer ambaye jana alisaini mkataba wa miaka mitatu wa kuitumikia Inter Milan amesema lengo kubwa alilonalo kwa sasa ni kuhakikisha klabu hiyo inapambana vyema kwa msimu huu na kumaliza wakiwa katika nafasi za juu katika msimamo wa ligi, ambazo zitawawezesha kucheza michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya msimu wa 2017/18.

Amesema suala hilo ni kubwa sana kwake kutokana na kuamini kwamba, endapo Inter Milan itarejea kwenye mshike mshike wa michuano mikubwa barani Ulaya itakuwa na kila sababu ya kuwavutia wachezaji wazuri na wenye hadhi ya kupambana wakati wote.

Meneja mpya wa klabu ya Inter Milan Frank de Boer

Hata hivyo De Boer ambaye amechukua nafasi ya Roberto Mancini ambaye usiku wa kuamkia juzi alilazimika kuondoka klabuni hapo kufuatia mambo kumuendea kombo msimu uliopita pamoja na kwenye michezo ya maandalizi ya msimu huu, amesisitiza suala la kutokua tayari kumuuza mshambuliaji kutoka nchini Argentina Mauro Emanuel Icardi Rivero.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 23 amekua katika rada za baadhi ya klabu za barani Ulaya hususan za nchini England (Chelsea na Arsenal) katika kipindi hiki cha usajili wa majira ya kiangazi.

Meneja huyo kutoka nchini Uholanzi amesema atahakikisha Icardi anaendelea kusalia klabuni hapo kutokana na kuamini bado anahitajika katika mipango yake ambayo itaisaidia Inter Milan kufikia lengo la kufanya vyema msimu wa 2016/17.

Uongozi Wa Simba Watoa Shukurani, Waipiga Kijembe Yanga
Arsene Wenger Amnyatia Wilfried Bony