Meneja wa klabu ya Chelsea, Frank Lampard huenda akabadili mpango wa kuwaachia wachezaji Willian na Olivier Giroud, ambao mwishoni mwa msimu huu watakua wachezaji huru baada ya mikataba yao kumalizika.
Mikataba ya wawili hao inatarajiwa kufikia kikomo Juni 30, lakini Lampard amesema anahitaji kuendelea kuwa na uimara wa kikosi chake na hafikirii kumuachia mchezaji yeyote.
Lampard anafikiria kuanza mazungumzo na wachezaji hao wawili ambao tayari wameshaanza kutajwa kwenye mipango ya usajili ya baadhi ya klabu za ndani na nje ya England.
“Tuna wachezai wenye hadhi kubwa ya kupambana, sitegemei kuona yeyote anaondoka kwenye kikosi changu, nahitaji kuwa nao wote kwa msimu ujao,” alisema Lampard alipohojiwa na Sky Sports.
“Wachezaji ambao mikataba yao ipo ukingoni, klabu itaanza utaratibu wa kufanya nao mazungumzo, na nina matumaini mambo yatakua mazuri,
“Kila mmoja anatamani kuiona Chelsea ikiendelea kuwa na kikosi kama ilivyo msimu huu, nina matarajio makubwa na kila mchezaji aliye kikosini kwa sasa na kila mmoja ana nafasi yake pale ninapomuhitaji kwa michezo husika.”
Tayari Williams alianza kuhusishwa na mipango ya kuwania na klabu za jijini London Arsenal na totenham Hotspurs, pia klabu ya Liverpool nayo ilitajwa kwenye mpango huo.