Kocha wa Mabingwa wa Soka nchini England Pep Guardiola anamtolea macho kiungo wa FC Barcelona, Frenkie de Jong, baada kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwania saini ya Declan Rice.
Lakini, FC Barcelona itahitaji Pauni 90 milioni, ambazo Guardiola alikuwa tayari kutoa kwa ajili ya Rice, kabla ya kujiondoa na kuipa mwanya Arsenal.
Uongozi wa Man City umeonyesha nia ya kusajili kiungo mwingine atakayeziba pengo la Ilkay Gundogan, ambaye alitimkia Barcelona.
Guardiola alimpotezea Rice baada ya West Ham kuongeza dau kubwa zaidi ya ofa aliyoandaa na kuiachia Arsenal balaa hilo, ikiwa ipo katika hatua za mwisho kumsajili wa Pauni 105 milioni.
Guardiola alipanga kumsajili De Jong 2019, kabla ya Mholanzi huyo hajakubali kusaini mkataba mrefu na Barcelona, lakini Guardiola aliendelea kumkubali.
De Jong alikuwa chaguo namba moja wa kocha Erik ten Hag, hata hivyo wakashindwa kumsajili kwa sababu kiungo huyo aligoma na kusisitiza hana mpango wa kuondoka Camp Nou.
Aidha, De Jong anaelewa Barcelona ipo tayari kumuuza kwa fedha nyingi kwa ajili ya kuongeza kipato, kwani hali yao ya kiuchumi si nzuri.
De Jong anapokea mshahara wa Pauni 400,000 kwa wiki na amebakiza mkataba wa miaka mitatu wa kuitumikia Barcelona.
Ingawa kocha wa klabu hiyo Xavi amekuwa akilinda uhamisho huu usifanyike kwa sababu ni mchezaji muhimu kwenye kikosi chake, Guardiola amepanga kuwasailiana na uongozi wa Barcelona.
Xavi aliweka wazi kuhusu hatima ya De Jong mwaka jana, akisema: “Amenieleza ukweli, anataka kubaki hapa na hakuna mashaka kuhusu hilo, De Jong ni mchezaji wetu na nina furaha kutokana na kiwango chake, yupo katika nyakati nzuri kama wachezaji wenzake.”