Baada ya ushindi muhimu wa mabao 3-1 dhidi ya mahasimu wao wakuu, Ashanti United, katibu mkuu wa klabu ya Friends Rangers, Kheri Mzozo ameibuka na kutamba kuwa hesabu na muujiza vipo upande wao katika mbio za kupanda Ligi Kuu msimu ujao.

Kwa ushindi huo, Friends Rangers ilifufua matumaini ya kupanda Ligi Kuu msimu huku zikiwa zimebaki mechi mbili kufikia tamati.

Katika mahojiano na Soka360, Mzozo amedai kuwa licha ya kuwa nyuma ya African Lyon, Ashanti United na KMC ana amini muujiza pamoja na hesabu za kupanda ligi kuu msimu ujao zipo upande wao.

“ Mechi yetu dhidi ya Ashanti ilikuwa kama fainali, wangeshinda wangekuwa na asilimia tisini ya kupanda. Friends tungefungwa au kutoka sare tungetoka kwenye mbio za kupanda Ligi Kuu”

“ Wanaoongoza hawajatupita sana. Uzuri ni kwamba African Lyon na Ashanti watacheza wao kwa wao, pia Ashanti hajacheza na KMC. Kwa hio Ashanti ana mechi mbili ngumu dhidi ya watu wanaopigania kupanda.

“ Tunashukuru tumefufua matumaini yetu. Mechi ijayo tunacheza na CDA, mechi ngumu sana kuliko zote kwa kuwa CDA anapigana kujinasua mkiani. CDA wanashinda na Polisi Dar wasishuke daraja, kwa hio itakuwa mechi ngumu sana kuliko ya Ashanti”

African Lyon inaongoza msimamo wa kundi A baada ya kuichapa Polisi Dar na kufikisha pointi 23. Ashanti United imebakiwa na pointi 22 baada ya kufungwa na Friends Rangers. KMC ina pointi 21 katika nafasi ya tatu huku Friends Rangers ikishika nafasi ya nne kwa pointi 20.

Timu zote zimebakiza mechi mbili katika mbio za kuamua nani anapanda Ligi Kuu msimu ujao kutoka Kundi A.

Klopp: Liverpool Jengeni Imani Na Maamuzi Yangu
Arsene Wenger Aanza Kuwazungumzia FC Barcelona