Shirikisho la Soka Nchini Uganda ‘FUFA’ limeusogeza mbele Mchezo wa Ligi Kuu nchini humo kati ya Arua Hill SC dhidi ya Vipers SC.
Mchezo huo ulipangwa kuchezwa kesho Machi Mosi, katika Uwanja wa Green Light mjini Arua, lakini FUFA wamechukua maamuzi ya kuusogeza mbele, ili kutoa nafasi kwa Vipers SC kujiandaa kuivaa Simba SC katika mchezo wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Afrika.
Vipers SC itacheza ugenini Dar es salaam-Tanzania Jumanne (Machi 07) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikihitaji ushindi ili kufufua matumaini ya kusonga mbele, katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Mchezo uliopita Vipers SC iliikaribisha Simba SC nchini Uganda, lakini ilipoteza kwa kufungwa 0-1, matokeo ambayo yalifufua matumaini kwa Mnyama ya kusonga mbele.
Hadi sasa Vipers SC inamiliki alama moja baada ya kupata sare ya 0-0 dhidi ya Horoya AC, lakini inaburuza mkia wa Kundi C, ikitanguliwa na Simba SC yenye alama tatu.
Horoya AC inashika nafasi ya pili kwa kuwa na alama nne, huku Raja Casablanca ikiongoza msimamo wa Kundi C ikiwa na alama tisa.