Mwishoni mwa juma lililopita, michezo ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa mwaka 2017, zilihitimishwa rasmi katika viwanja vya miji mbalimbali barani humo na kushuhudia timu za mataifa 15 zikifuzu na kuungana na taifa mwenyeji Gabon.

Kufuzu kwa mataifa hayo 15 sambamba na taifa mwenyeji katika fainali za kombe la Afrika za mwaka 2017, kumeanza kuwapa wakati mgumu baadhi ya mameneja wa klabu za ligi mbambali barani Ulaya na kwingineko.

Katika ligi ya nchini England ambayo imekua ikifuatiliwa na mashabiki wengi duniani, kuna baadhi ya klabu zitalazimika kuwaachia wachezaji wao ambao mataifa yao yamefuzu kuelekea nchini Gabon tayari kwa fainali hizo ambazo zitaanza rasmi mapema mwakani.

Arsenal

Wanatarajiwa kumkosa kiungo wao kutoka nchini Misri Mohamed Elneny, ambaye tayari ameshaitumikia timu yake ya taifa katika michezo 44. Elneny alifanikiwa kucheza michezo yote ya kuwani kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika za mwaka 2017 kupitia kundi G ambalo lilikua na timu za Tanzania, Nigeria pamoja na Chad ambayo iliamua kujitoa kufuatia sababu za kukosa fedha.

Bournemouth

Wanatarajia kumkosa mshambuliaji wao wa pembeni kutoka Ivory Coast Max Gradel ambaye ameshaichezea timu yake ya taifa katika michezo 44 na kufunga bao moja.

Crystal Palace

Wanatarajia kumkosa kiungo mshambuliaji kutoka nchini Mali Bakary Sako pamoja na beki wa pambeni kutoka nchini Senegal Pape Souare.

Everton

The Toffees wanatarajia kuwa wahanga wakubwa katika fainali za AFCON 2017, kufuatia kuwa na wachezaji zaidi ya wawili ambao watawakosa katika kipindi cha mwanzoni mwa mwaka ujao.

Idrissa Gueye na Yannick Bolasie wanatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha timu ya taifa ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Oumar Niasse wa Senegal pamoja na Arouna Kone wa Ivory Coast.

Hull City

Ahmed Elmohamady anatarajiwa kuwa sehemu ya wachezaji watakaounda kikosi cha timu ya taifa ya Misri. Lakini hakuwahi kucheza katika michezo yote ya hatua ya kusaka nafasi ya kufuzu kwa fainali za AFCON 2017, licha ya kubahatika kuitumikia timu yake ya taifa katika michezo 71.

Leicester City

Riyad Mahrez pamoja na Islam Slimani wana nafasi kubwa ya kuitwa katika kikosi cha timu ya taifa ya Algeria, Sambamba na Daniel Amartey na Jeffrey Schlupp huenda wakatajwa kwenye orodha ya wachezaji wa kikosi cha Ghana, huku kukiwa na mashaka ya kumkosa Even Yohan Benalouane wa Tunisia.

Liverpool

Sadio Mane ana nafasi kubwa ya kukosa michezo ya ligi kuu ya soka nchini England mwanzoni kwa mwaka ujao, kufuatia kiwango chake kuwa chagizo kwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Senegal, huku Joel Matip akitazamiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Cameroon, japo hakuwahi kuitwa tangu mwezi Septemba mwaka 2015.

Manchester City

Meneja Pep Guardiola atalazimika kusaka mbinu mbadala za kuziba pengo la kiungo Yaya Toure.

Toure anatarajia kuzitumia fainali za AFCON 2017 kama sehemu ya kuendeleza mazuri aliyoyafanya wakati wa fainali za mwaka 2015 ambapo Ivory Coast walitawazwa kuwa mabingwa.

Manchester United

Wanatarajiwa kumkosa mchezaji mmoja ambaye ni Eric Bailly anayeitumikia timu ya taifa ya Ivory Coast. Tayari ameshaitwa mara 14 katika timu hiyo.

Southampton

Kiungo mshambuliaji aliyesajiliwa klabuni hapo wakati wa majira ya kiangazi Sofiane Boufal huenda akawa mchezaji pekee ambaye atakosekana katika kikosi cha The Saint. Sofiane Boufal ni raia kutoka nchini Morocco.

Stoke City

Hatua ya kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Man City Wilfried Bony, imeilazimu klabu hii kuongeza idadi ya wachezaji ambao watakosekana kwenye kikosi chao mwanzoni mwa mwaka 2017.

Bonny ni mshambuliaji wa kutumainiwa kwa sasa katika kikosi cha Ivory Coast na katika harakati za kurejea nyumbani Afrika mwezi Januari atajumuika na waafrika wenzake kutoka Stoke City kama Mame Biram Diouf wa Senegal pamoja na Ramadan Sobhi wa Misri.

Sunderland

Klabu hii inayonolewa na meneja David Moyes, nayo ni miongoni mwa watakaoathirika mwezi Januari mwaka 2017 kufuatia uwepo wa Lamine Kone wa Senegal, Wahbi Khazri wa Tunisia, Didier Ndong wa Gabon na Papy Djilobodji wa Senegal.

Watford

Watamkosa Nordin Amrabat wa Morocco sambamba na Adlene Guedioura (Algeria) pamoja na Brice Dja Djedje (Ivory Coast).

West Brom

Wanatarajia kumkosa Allan Nyom ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuitwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Cameroon. Mpaka sasa ameshaichezea timu ya taifa katika michezo 14, na mara kadhaa alijumuishwa kwenye kikosi kilichokua kikisaka nafasi ya kushiriki fainali za AFCON 2017.

West Ham

Watamkosa Sofiane Feghouli (Algeria), Cheikou Kouyate pamoja na Diafra Sakho (Senegal). Mwingine atakaekosekana ni Andre Ayew (Ghana).

Lionel Messi Yu Mashakani, Kuwakosa Alaves, Celtic
Baada Ya Kuikacha AFCON 2017, Chad Yaibukia Ufaransa