Atanga ‘Ngoma’ Schneider kutoka Cameroon, ameachia video ya wimbo wake mpya, All Les Day. Mkito huo umetayarishwa na Dijay Karl, aliyefanya naye kazi kwa miaka mingi.
‘All les Day, ukimaanisha ‘Kila Siku’, ni wimbo wa hip hop uliopambwa na mtindo wa Trap iliyonakishwa na mitindo asili ya uchanaji katika viunga vya mitaa maarufu ya Cameroon.
Mkito huo upa una vionjo vya mtindo wa Jwe’te ambao ni mchanganyiko wa muziki wa asili wa kabila la Ngemba ambavyo vinasikika kwa mara ya kwanza kwenye wimbo. Amesema vionjo hivyo vitasikika zaidi kwenye nyimbo zake zijazo. Pamoja na kutumia Pidgin English (Kiingereza kizungumzwacho Cameroon), Ngoma ametumia Kifaransa pamoja na kabila na Ngemba kwenye wimbo huu. Video yake imeongozwa na Shamak Allharamaji.
Ngoma si mgeni kwenye masikio na macho ya mashabiki wa muziki wa Tanzania. Mwaka jana akiwa na wimbo wake maarufu, Mangosi, alifanya ziara ya vyombo vya habari jijini Dar es Salaam katika vituo vya redio na TV vikiwemo Clouds TV, East Africa Radio, EFM, Times FM na Magic FM.
Katika ziara yake hiyo, Ngoma alifanikiwa kurekodi collabo na Ray Vanny katika studio za Surprise Music chini ya producer Rash Doni, huku mdundo na ukamilishaji wa wimbo ukifanywa na Dijay Karl. Amepanga kuachia wimbo huo mapema mwakani wakati wa shamrashamra za Kombe la Mataifa ya Afrika. Pia Ngoma amesema baada ya kuachia video takriban nne, ataachia album yake inayosubiriwa kwa hamu, G.O.A.T(Greatest of All Time).