Mbunge wa Jimbo la Ulanga Mkoani Morogoro, Salim Alaudin Hasham amewataka Vijana waendesha Bodaboda Wilayani humo, kuunda vikundi kwaajili ya kuchangamkia fursa mbalimbali za kimaendeleo zilizopo, ili waweze kukuza uchumi wao.
Mbunge Salim ameyasema hayo, wakati wa kukabidhi reflector kwa bodaboda hao wapatao 324 ili kuwafanya watambulike rasmi na kuepusha vitendo vya kihalifu vinavyofanywa na watu wanaojifanya ni bodaboda katika Wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Kitengo cha Usalama Barabarani Wilaya ya Ulanga, Joseph Isagala amemshukuru Mbunge Salim Hasham kwa kuwapatia bodaboda reflector hizo na amewataka kujitokeza kwa wingi pindi mafunzo maalum ya sheria za usalama Barabarani yatakapokuwa yanatolewa.
Awali, Viongozi wa Bodaboda hao, Elia Tirani na Clement liyengejele wamemshukuru Mbunge kwa msaada huo na wamemuahidi kuwahamasisha vijana kushiriki kwa wingi mafunzo ya sheria za Barabarani, ili wapate leseni ambazo zitawaepusha kukamatwa mara kwa mara na Askari.
Aidha, Viongozi hao pia wametumia fursa hiyo kumuomba Mbunge huyo kuwawezesha mikopo ya Pikipiki, ili waweze kujikwamua kwani pikipiki walizonazo kwasasa si zao hivyo zinawafanya kushindwa kujiinua kiuchumi ipasavyo.