Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainabu Chaula ametoa rai kwa vijana kutunza maadili ya nchi na kuwa na matumizi sahihi ya teknolojia kwa maslahi mapana ya nchi kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano kutafutia fursa za kiuchumi na kupata taarifa sahihi za biashara, elimu na afya
Dkt. Chaula amezungumza hayo wakati akizindua mafunzo ya siku nane ya programu ya HUAWEI Tanzania iitwayo Seeds for the future jijini Dodoma Septemba 3, 2021
Ameizungumzia programu hiyo kama fursa ya kuongeza uwezo na kukuza vipaji kwa vijana wanataaluma wa TEHAMA kupitia kampuni ya HUAWEI ambao ni wadau muhimu wa Sekta ya Mawasiliano katika kuweka mazingira wezeshi ya kukuza TEHAMA nchini
Amesema kuwa programu hiyo kwa mwaka huu inawahusisha vijana 50 ambao ni wanafunzi wa taasisi za elimu ya juu watakaopata nafasi ya kujifunza teknolojia za kisasa za TEHAMA zitakazokuza uwezo na ubunifu wao na kuwaletea faida wao binafsi, Taifa na jamii kwa ujumla
Aidha, Dkt. Chaula amesema kuwa fursa nyingi zinapatikana kupitia TEHAMA na kati ya vijana 50 watakaopatiwa mafunzo hayo vijana 40 ni wasichana kitu ambacho kinatia moyo na kutoa hamasa kwa vijana hasa kutokana na ushuhuda wa moja ya wanufaika wa programu hiyo Bi. Emilina Masanja kutoka chuo kikuu cha Mzumbe aliyesema kupitia TEHAMA amekuza biashara yake kwa kuongeza wigo wa wateja ambao wengine wapo nje ya nchi
Naye Profesa Albino Tenge akimwakilisha Makamu Mkuu wa Chuo kikuu cha Dodoma Profesa Faustine Bee amesema kuwa chuo hicho kina ndaki ambayo inafundisha taaluma ya teknolojia ya habari na mawasiliano inayoitwa CIVE, hivyo programu ya HUAWEI Tanzania ya Seeds for the Future inatoa hamasa kwa vijana wanaochukua kozi za TEHAMA kwa kuwapa nafasi ya mafunzo kwa vitendo na pia inawezesha vijana hao kuweza kujiajiri na kuajirika
Kwa upande wa Mkurugenzi Msaidizi wa HUAWEI Tanzania Tom Tao amesema kuwa mafunzo hayo ni yameanza kutolewa mwaka 2016 kwa kuchagua wanafunzi 10 wa TEHAMA wanaofanya vizuri kutoka katika taasisi za elimu ya juu kwa kuwapatia mafunzo ya teknolojia za kisasa katika TEHAMA nchini China na pia kujifunza utamaduni wao
Ameongeza kuwa kutokana na changamoto za UVIKO 19, kuanzia mwaka jana mafunzo hayo yamekuwa yakitolewa kwa njia ya mtandao na idadi ya wanafunzi hao kuongezeka kutoka 10 hadi kufikia wanafunzi 50 ambapo mpaka sasa jumla ya wanafunzi 150 wamenufaika na programu hiyo