Mkurugenzi wa taasisi ya ‘Karibu Tanzania Organization’ (KTO,) Maggid Mjengwa amewaasa wanawake vijana kutumia fursa ya vyuo vya Maendeleo ya Wananchi (FDCs) vilivyopo kote nchini kupata elimu ya sekondari, stadi za maisha na elimu ya ujasiriamali ili kuweza kunufaika  kupitia miradi mbalimbali ya kiuchumi inayotangazwa na Serikali.

Ameyasema hayo wakati wa ufunguzi mafunzo maalum ya siku 5 kwa waratibu wa mafunzo,  walezi wa wasichana na walimu wakuu wa vyuo vya Maendeleo ya Wananchi 13 vinavyotekeleza programu ya Elimu Haina Mwisho inayowahusu wasichana waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito na ndoa za utotoni pamoja na umasikini.

Mjengwa amesema kuwa kwa sasa jamii imeamka na hii ni kutokana na mkazo wa Elimu hasa kwa wanawake uliotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hasssan ambapo Karibu Tanzania Organization’ (KTO,) ikishirikiana na serikali katika kuhakikisha mradi wa wa FDCs inawanufaisha vijana na kuweza kujiinua kiuchumi mara baada ya kupata mafunzo katoka vyuo hivyo.

”Vijana wengi wamekuwa wakinufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendelea kote nchini, vijana wamekuwa wakipata fursa za ufundi umeme na uchomeleaji katika miradi mikubwa ikiwemo REA na mradi wa uchimbaji wa madini ya Nickel mkoani Kagera…fursa hii ya kupata Elimu na ujuzi itumiwe vyema na vijana katika kujenga Taifa imara.” Amesema Mjengwa

Kuhusiana na mafunzo hayo Mjengwa amesema, ongezeko la vyuo 13 zaidi kutoka 41 na kufikia 54  ni kutokana na agizo la Serikali la kutaka vyuo vyote kudahili wanafunzi wa kundi hilo kupitia programu ya Elimu Haina Mwisho kuanzia Januari mwaka huu.

”Kupitia agizo hili tukaona ni vyema kukutana na walimu, waratibu na walezi wa vyuo hivi 13 na kuwapatia mafunzo ya msingi,ujuzi, msaada ya kisaikolojia na changamoto za kukabiliana katika mchakato mzima wa kufanikisha safari ya mabinti wanaowahudumia.” Amesema Mjengwa

Ameeleza kuwa, mabinti wenye sifa za kukatiza masomo kwa sababu mbalimbali wakiwa vyuoni kwa miaka miwili  watasoma bila kulipa ada pamoja na kupata elimu ya sekondari na mafunzo ya ziada  ambayo ni  Elimu ya sekondari 50%, stadi za maisha 10%, ufundi na ujuzi 30% na Elimu ya ujasiriamali 10%.

”Wanafunzi wanachogharamia ni mahitaji binafsi ikiwemo nauli na mahitahi mengine ikiwemo taulo za kike ambazo  bado ni changamoto na tunaangalia wadau waweze kusaidia eneo hilo…..Kuhusiana na chakula na malazi vyote vinagharamiwa na Serikali katika kuhakikisha kila mwanamke kijana anatimiza ndoto zake kielimu na kiuchumi.” Amesema Mjengwa

Kuhusiana na mabinti wa kike walio na watoto, Mjengwa amesema wanaweza kunufaika na programu hiyo kwa kuwa vyuo 34 kati ya 54 vina vituo vya malezi na makuzi ya watoto ambavyo watoto watapata huduma ya malezi katika vituo hivyo bure. 

Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi vilivyoshiriki mafunzo hayo ni Arnatouglu FDC’s- Dar es Salaam, Bariadi FDCs- Simiyu, Buhangija FDCs- Shinyanga, Chala FDC’s – Sumbawanga, Chilala FDC’s – Lindi, Gera FDC’s- Kagera, Kilosa FDC’s- Morogoro, Kisangwa FDC’s- Bunda, Msingi FDC’s- Singida, Musoma FDC’s- Mara, Nandembo FDC’s- Tunduru, Tarime FDC’s- Mara na Ulembwe FDC’s kutoka Njombe.

Rais wa Ukraine asema NATO walimtosa, ‘walijua tutapigwa’
Rais Samia aeleza walichozungumza na Mbowe Ikulu