Kiungo wa Hull City ya England, Ryan Mason, amelazimika kustaafu soka ikiwa imepita mwaka mmoja tangu alipovunjika fuvu la kichwa kwenye mechi ya ligi kuu soka England dhidi ya Chelsea.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 aligongana na mlinzi wa kati wa Chelsea, Gary Cahill uwanjani Old Trafford Januari 22 mwaka jana na akafanyiwa upasuaji ambapo alikaa siku nane katika Hospitali ya Saint Mary Jijini London akipigania uhai wake.
Mason amethibitisha kwenye taarifa yake akisema kustaafu kwake kumetokana na ushauri wa madaktari ambao walipigana kuhakikisha anarejea uwanjani, lakini wamemtaka kuachana na soka kutokana na aina ya majeraha aliyopata.
Mwanasoka huyo ametoa shukrani kwa familia yake, mpenzi wake Rachel na ndugu jamaa na marafiki kwa kuwa naye bega kwa bega katika kipindi chote alichokuwa akihangaikia afya yake.
Hull City imetoa taarifa ikisema klabu imeumizwa na kitendo cha Mason kustaafu kwani alikuwa mchezaji kijana mwenye ndoto kubwa ya kuisaidia klabu.