Mwanariadha Gabriel Geay ameeleza namna alivyopambana na magwiji wa Marathoni wa Dunia hadi kuibuka mshindi wa Medali ya fedha kwenye mbio za Boston Marathon Jumatatu iliyopita.
Mtanzania huyo alimaliza wa pili akitumia saa 2:06:04 akiachwa kwa sekunde tisa na bingwa raia wa Kenya, Evans Chebet aliyetumia saa 2:05:54.
Mwanariadha mwenye kasi zaidi duniani kwenye marathoni, Eliud Kipchoge alimaliza wa sita akitumia saa 2:09:23 katika mbio hizo kongwe za pesa nchini Marekani.
Geay aliiambia amesema alianza kuutengeneza ushindi wake katika Kilomita ya 32 alipompiku Kipchoge na kuona kumbe inawezekana.
“Ilikuwa ni mbio zenye presha kutokana na wakimbiaji tuliokuwa pale, lakini maandalizi niliyofanya, kujituma na jitihada ndizo zilinipa matokeo haya,” amesema
Amesema walipoanza mbio, wengi walikuwa wakimtazama Kipchoge kutokana na rekodi yake, lakini katika kundi la kwanza walikwenda sambamba hadi walipofika Kilomita ya 32 wakaanza kuachana.
“Pale ndipo nilimpita Kipchoge, tukabaki kwenye kundi ambalo lilitoa bingwa, Chebet tulikwenda naye sambamba hadi kilomita ya 40 ndipo alipoongeza kasi na kumaliza bingwa,” amesema Geay
Amesema kulikuwa na changamoto nyingi za upinzani, na kila mmoja kwenye mbio hizo alipambana ili kufanya vizuri na Chebet kwa kuwa ni bingwa mtetezi alitumia mbinu ya kutoka na kuongeza mwendo wakiwa wamesalia na Kilomita 2 kumaliza mbio.
“Nilimfuata, tageti yangu ilikuwa ni dhahabu, lakini alimaliza wa kwanza kwa sekunde chache mbele yangu,” amesema Geay ambaye ni mara ya pili anachuana kwenye mbio hizo ambazo bingwa aliondoka na Shilingi Milioni 351.
Akizungumzia mipango yake baada ya Boston, kocha wa Geay, Thomas Tlanka amesema kabla ya mashindano ya Dunia, atachuana kwenye mbio za kimataifa za nusu marathoni.
“Bado hatujapanga ni wapi, lakini atakimbia nusu marathoni ili kuimarisha kasi yake,” amesema