Meneja wa Mshambuliaji wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Meddie Kagere, ameibuka na kuonesha yupo tayari kumuona mchezaji wake akiondoka klabuni hapo na kuelekea upande wa pili (Young Africans).
Patrick Gakumba, meneja wa mshambuliaji huyo ambaye msimu huu amekua na wakati mgumu wa kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Simba SC, ameibuka na kuwataka Young Africans kuwa wazi kama wanahitaji huduma ya mchezaji wake.
Gakumba ambaye majuma mawili yaliyopita aliingia kwenye mgogoro na baadhi ya Mashabiki na Wanachama wa Simba SC, kufuatia tuhuma alizomuangushia kocha Didier Gomes, akidai alishindwa kumtumia mchezaji wake wakati wa mchezo wa mkondo wa pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Kaizer Chiefs hatua ya Robo Fainali amekaririwa akisema “Yanga njooni tuzungumze.”
Kauli hiyo imemaanisha wazi hayupo tayari kuona Kagere akiendelea kuitumikia Simba SC kwa msimu ujao, hata kama Uongozi wa klabu hiyo utaonesha nia ya kumsainisha mkataba mpya, katika kipindi hiki ambacho kuna sekeseke kubwa la usajili.
“Kuhusu mkataba wake na Simba SC, utafikia ukingoni baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu msimu huu 2020/21, baada ya hapo atakuwa mchezaji huru. Kama Yanga wanahitaji huduma yake tunawakaribisha kuzungumza” amesema Gakumba.
Meddie Kagere alisajiliwa Simba SC misimu miwili iliyopita akitokea Gor Mahia ya Kenya, na kwa wakati wote amekua tishio katika orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu, akichukua tuzo hiyo mara mbili mfululizo.
Kwa msimu huu 2020/21 Kagere anashika nafasi ya tatu katika orodha ya wapachika mabao, akiwa na mabao 11, akitanguliwa na John Bocco mwenye mabao 13, huku nafasi ya kwanza ikishikwa na mshambuliaji wa Azam FC Prince Dube mwenye mabao 14.