Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amezindua ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Arusha mjini katika eneo la Njiro kontena. Shughuli ambayo ilihidhuriwa na mamia ya wakazi wa Jiji hilo.
Akizungumza na wananchi hao Gambo alisema “Nina furaha sana kushuhudia tukio hili litakaloacha alama katika maisha ya watu wetu wa Arusha,kwani wakati wa kampeni Mhe Rais Magufuli aliahidi na tunatekeleza kwa vitendo.”
Hospitali hiyo inatarajiwa kuhudumia wakazi zaidi ya laki nne kutoka wilayani humo na maeneo ya jirani ili kupunguza idadi ya wagonjwa wanasababisha hospitali ya mkoa ya Mount Meru kuelemewa.
Vile vile Gambo anasema kwa sasa mapato yanayokusanywa na Jiji la Arusha kwa mwaka bado hayatoshelezi  hata kulipa mishahara ya watumishi wake na kwa maana hiyo ni muhimu kuweka mifumo thabiti ya ukusanyaji wa mapato jijini humo.
“Jiji la Arusha mapato yake ya ndani kwa mwaka hayazidi bilioni 12 na mishahara pekee ya watumishi wa halmashauri ni zaidi ya bilioni 40, sasa hapo ukilipa tu mishahara hela yote inakwisha na bado unakua na deni, sasa hata fedha za maendeleo zitatoka wapi zaidi ya kutegemea hela zinazoletwa na Magufuli?? Gambo alihoji.
Ujenzi wa Hospitali ya wilaya ya Arusha kwa awamu ya kwanza unafanyika katika moja ya maeneo ya wazi yaliyo kuwa yakimilikiwa kinyemelela na baadhi ya wajanja wachache na kwa sasa ujenzi umeanza ambao utagharimu kiasi cha shilingi milioni 500 hii ikiwa ni jengo la Ghorofa moja kwa ajili ya wagonjwa wa nje.
Naye mkurugenzi wa Jiji la Arusha Athuman Kihamia alimshukuru Mhe Gambo kwa kuweza kulipigania eneo hilo mpaka limeweza kurudi kwenye mikono ya wananchi.
“Kwakweli kama sio jitihada zako eneo hili lilishaondoka mikononi mwetu hivyo kwa niaba ya wananchi wa Arusha ninakushukuru sana, pia nikuahidi tutazingatia ushauri wako wa kulitumia eneo hili vizuri kwa kujenga majengo ya ghorofa kuanzia tano ili kulitumia eneo hili vizuri” alisema Kihamia.
Ujenzi wa Hospitali hiyo unatarajiwa kukamilika June mwaka 2018 ambapo zaidi ya wakazi laki 4 watapata huduma ya afya karibu na makazi yao tofauti na ilivyo.
Video: Waziri Mkuu atoboa siri hii kwa wananchi, "Mimi kama mtendaji mkuu wa Serikali..."
Magazeti ya Tanzania leo Desemba 24, 2017