Mpambano wa kukata na shoka uliokua unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka karibu wote duniani kati ya Manchester City dhidi ya Manchester United umeahirishwa.

Mpambano huo wa michuano ya International Champions Cup ambao ulipaswa kuchezwa mjini Beijing umesogezwa mbele kutokana na hali ya uwanja kutokua nzuri.

Taarifa iliyotolewa katika tovuti ya klabu ya Man Utd, imeeleza kwamba sehemu ya kuchezea ya uwanja Bird’s Nest imeathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya hewa ya mjini Beijing hivyo imeshauriwa mchezo huo usichezwe hii leo.

“Kutokana na hali ya hewa na unyevu unyevu ya mjini Beijing, waratibu wa michuano ya International Champions Cup, wamelazimika kuufuta mchezo na ratiba mpya inasubiriwa,” ilieleza taarifa hiyo

Meneja wa Man Utd, Jose Mourinho mwishoni mwa juma lililopita alilalamika mbele ya waandishi wa habari kuhusu mazingira ya sehemu ya kuchezea ya uwanja wa Bird’s Nest, kwa kusema haikua rafiki kwa wachezaji wake.

“Nafikiri mji wa Beijing unakosa bahati ya kuwa na michezo mikubwa ya soka, kutokana na hali yake ya hewa.

“Hali za Afya kwa wachezaji wangu ni muhimu kuliko jambo lolote hivyo sijapendezwa na mazingira ya sehemu ya kuchezea ya uwanja ule. Alisema Mourinho.

Mchezo wa hii leo ulitarajiwa kuwakutanisha Jose Mourinho na Pep Guardiola kwa mara ya kwanza tangu walipoachana katika ligi ya nchini Hispania wakiwa na klabu za Real Madrid na FC Barcelona.

Wawili hao kwa msimu huu watakua nchini England wakiviongoza vikosi  vya klabu nguli za mjini Manchester.

Video: Dhamira ya Rais Magufuli Kuhusu Serikali Kuhamia Dodoma
Kolo Toure: Nitapambana Wakati Wote