Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Gamondi amewataka Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kutarajia mazuri zaidi ya msimu uliopita, hivyo wanapaswa kuwa watulivu na kumpa ushirikiano wakati wote.
Gamondi ambaye aliwasili nchini usiku wa Ijumaa (Julai 7), anatarajia kuanza kukinoa kikosi cha Young Africans kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ pamoja na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema anategemea kukiandaa vizuri kikosi chake ili kuonesha soka safi na kupata mafanikio makubwa, huku akitarajia kutetea mataji yote walioyatwaa msimu uliopita.
Hata hivyo Kocha Gamondi amekiri ana kazi kubwa ya kufanya ili kuvuka mafanikio ya Kocha aliyemtangulia Nasreddine Nabi.
“Natarajia kuwa na timu nzuri na bora na napenda kuwa na wachezaji ambao ni waumini wa kucheza mpira natamani kuona timu yangu inacheza mpira mzuri kuanzia nyuma na kwenda mbele, soka la kuchangamka,”amesema Gamondi
Amesema anafahamu anatazamwa na kila mwanasoka kuona atafanya nini katika klabu hiyo, hivyo ana kila sababu ya kukaa na wachezaji wake mapema.
Amesema ameutaka uongozi kuwarudisha wachezaji kambini mapema ili aweze kupata muda wa kuanza kuwazoea.
“Bado sijapata nafasi ya kukaa na wachezaji lakini nimeomba nafasi hiyo ili kuweza kuanza kambi mapema mimi ni mgeni kikosini nahitaji kuona ubora wa kila mchezaji ili nifahamu nafanya kazi na watu wa aina gani,”amesema.
Tayari Uongozi wa Young Africans umeshaweka wazi kuwa, kambi ya timu yao itakua Avic Town, Kigamboni nje kidogo ya jijini Dar es salaam.