Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema kuwa amefurahishwa na hatua ya mchezo wao wa Raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Al Merreikh ya Sudan kuchezwa nchini Rwanda kutokana na ukaribu wa nchi hizo mbili.

Al Merreikh wamethibitisha mchezo huo wa Mkondo wa Kwanza utachezwa Septemba 16 kwenye Uwanja wa Kigali Pele nchini Rwanda na siyo Morocco kama walivyotaka kufanya hivyo kabla ya Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ kukataa ombi hilo.

Akizungumza jijini Dar es salaam, Kocha huyo amesema faida ambayo wataipata kwa mchezo huo kuchezwa Rwanda ni wachezaji kutochoka kwa safari ndefu, lakini watatumia saa chache wakiwa safarini tofauti na mchezo huo ungechezwa Morocco ambapo wangetumia zaidi ya saa 48.

Tunaweza kufanya mazoezi hapa na kisha tukatumia saa chache kwenda Rwanda, hiyo ni faida kubwa kwetu sababu wachezaji hawatapata uchovu lakini faida nyingine ambayo ni kubwa mashabiki wetu wanaweza kusafiri kutupa sapoti,” amesema Gamondi.

Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema anatambua huo ni mchezo mgumu kwao kutokana na ubora na ukubwa wa wapinzani wao Al Merreikh, lakini wapo katika mazoezi kabambe kuhakikisha wanashinda vita hiyo na kufuzu hatua ya makundi.

Amesema kwa sasa wanachokifanya kwenye mazoezi yao ni kuwapa wachezaji wake mbinu zitakazowapa matokeo chanya kwenye mechi hizo mbili ambazo lengo laoni kuhakikisha wanacheza kwa kujituma ili kutimiza walichokikusudia.

Kwa mujibu wa uongozi wa Young Africans, msafara wa timu hiyo unatarajia kwenda nchini Rwanda Septemba 14 ukiwa na wachezaji wake wote wakiwemo wale waliopo kwenye timu zao za taifa hivi sasa.

Singida FG yaweka kambi Dar es salaam
Abiria andikeni majina sahihi wakati wa Safari - SSP Didi