Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Miguel Angel Gamondi amefunguka kuelekea mchezo wa Mzunguuko wanne wa Ligi Kuu utakaochezwa leo Jumatano (Oktoba 04) dhidi ya Ihefu FC itakayokuwa nyumbani katika Uwanja wa Highland Estate, mjini Mbarali mkoani Mbeya.

Young Africans itacheza mchezo huo wa kwanza ugenini tangu kuanza kwa msimu huu 2023/24, ikitangulia kucheza michezo mitatu Uwanja wa nyumbani Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam.

Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema anatambua ugumu wa mchezo huo, lakini amekiandaa vyema kikosi chake kuondoka na alama tatu muhimu, ambazo zitaendelea kuwaweka kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Gamondi amesema anatambua Ihefu FC ina kikosi kizuri ambacho kitatoa upinzani mkubwa dhidi ya kikosi chake baadae leo jioni, lakini anaamini maandalizi mazuri alioyafanya yatamuwezesha kuondoka kwa furaha katika Uwanja wa ugenini.

“Ihefu ni wagumu wanapokuwa kwao, tumejiandaa kupambana, kila mchezaji anatamani kufanya vizuri katika mchezo ili timu iweza kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo,” amesema.

Kwa Upande wa Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Zuberi Katwila, amesema kikosi chake kipo fiti kuikabili Young Africans na ana imani wachezaji wake watafuata maelekezo atakayowapatia.

“Tumefanya maandalizi ya mchezo huu, naamini tutafanya vizuri kwa kupambana ndani ya uwanja na pia tutakuwa na faida ya kutumia Uwanja wa nyumbani,” amesema.

Katika ligi hiyo msimu huu, Young Africans imeshinda mechi tatu, ikiifunga KMC mabao 5-0, JKT Tanzania (5-0) na Namungo (1-0).

Ihefu imeanza ligi kwa kusuasua baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Geita Gold (nyumbani), kabla haijaifunga Kagera Sugar 1-0 (nyumbani) na baadae ilifungwa na Mashujaa mabao 2-0 ugenini.

Pamoja na timu hiyo kushinda mechi moja pekee hadi sasa msimu huu, Young Africans itakuwa na kibarua kigumu kuifunga Ihefu katika uwanja huo kwani mara ya mwisho timu hizo kuvaana dimbani hapo, miamba hiyo kutoka Mbarali ilishinda 2-1.

Makali mapya bei za Mafuta zikizidi kupaa
Wawili mbaroni kwa kutengeneza Noti bandia