Kocha Mkuu wa Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara Young Africans Miguel Angel Gamondi amefichua siri ya ushindi mnono wa mabao 5-1 dhidi ya Simba SC, walioupata juzi Jumapili (Novemba 05), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.
Mabao mawili ya Maxi Nzengeli na matatu yaliyofungwa na Pacome Zouzoua, Kennedy Musonda na Stephane Aziz Ki, yalitosha kuipa Young Africans ushindi huo ambao uliipeleka kileleni mwa msimamo wa Ligi ikifikisha alama 21.
Akizungumzia matokeo hayo, Gamondi amesema hayakupatikana kwa bahati mbaya kwani timu yake ilijiandaa kuyapata kutokana na namna walivyofanyia kazi ubora na udhaifu wao na ule wa Simba SC.
“Unajua soka ni mchezo wa maandalizi. Ulichokiona uwanjani tulikifanya sana mazoezini kwetu na pale Uwanjani tulikwenda kuburudika. Tulitarajia kushinda kwa sababu tulijiandaa vyema na nilisema hivyo hata kabla ya mechi,” amesema Gamondi.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema kuwa aliamini kutawala eneo la kiungo kungekuwa silaha kubwa kuimaliza Simba SC na ndilo jambo lililotokea, akiwasifu viungo wake Pacome, Nzengeli na Aziz Ki ambao waliipoteza safu ya kiungo ya wapinzani wao.
“Niliisoma vyema Simba SC na kujua ubora na upungufu wao. Wako vizuri kwenye eneo la kiungo na sisi tuna watu bora eneo hilo,” amesema Gamondi.
“Nawaamini wachezaji wangu. Niliwaambia wasiwe na presha, bali wafanye kile wanachofanya kila siku mazoezini na hata kwenye mechi na nafurahi walinielewa na kufanya hivyo. Najivunia wao.”
Gamondi amesema kuwa kwa sasa nguvu na akili wanazielekeza katika mchezo dhidi ya Coastal Union, utakaopigwa kesho Jumatano (Novemba 08) katika Uwanja wa CCM Mkwakwani mjini Tanga.