Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi amesema kulingana na mfumo anaoutumia kila mchezaji anaweza kufunga mabao sio lazima mshambuliaji mwenye jukumu hilo.
Young Africans hadi sasa ameshacheza mechi tisa huku wakifunga mabao 26, Stephane Aziz Ki na Maxi Nzengeli wakiwa vinara wa kufunga ndani ya klabu hiyo kila mmoja akifunga mabao saba na manne yakifungwa na Pacome Zouzoua.
Mabao mawili yamefungwa na washambuliaji moja kwa Hafiz Konkoni na Clement Mzize na yaliyosalia yakifungwa na Mudathir Yahya na Dickson Job.
Gamondi amesema kuwa mipango yake katika kufundisha anawapa uhuru wachezaji wake wake hasa mwenye uwezo wa kutumia nafasi anaweza kufunga na sio lazima Mshambuliaji.
Gamondi amesema wachezaji wote wana kazi ya kupambania uwanjani ili kutafuta ushindi, lazima kila mtu kuwa makini kutumia vizuri nafasi zinazopatikana bila kujali anacheza nafasi gani.
“Mipango yangu kila mchezaji anatakiwa kutumia nafasi zinazopatikana akiwa sehemu nzuri kufunga anaweza anatakiwa kufanya jukumu hilo, kila mtu yupo huru kupambania timu inapata matokeo chanya.
“Ukiangalia mabao tuliyofunga mengi yamefungwa na viungo, washambuliaji hawajafunga mabao mengi, hii ni jinsi gani ninavyotaka kwa wachezaji wangu hasa katika kushirikiana katika kutimiza majukumu,” amesema Gamondi.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina ameongeza kuwa viungo wanafunga mabao mengi na mabeki watafanya hivyo kwa kuwa anawapa uhuru wa kufunga ili kuipa timu matokeo mazuri ili kufikia malengo yao.