Kocha Mkuu mpya wa Mabingwa Soka Tanzania Bara Young Africans Miguel Angel Gamondi, ameongea kwa mara ya kwanza akisema iwapo watashirikiana vizuri kufanya kazi kwa pamoja na uongozi, basi Wanachama na Mashabiki wa klabu hiyo wataendelea kufurahi kwani yeye ni Kocha mzoefu wa soka la Kiafrika kwa zaidi ya miaka 20 sasa.

Akizungumza akiwa nchini kwao Argentina, Kocha huyo aliyetangazwa rasmi juzi Jumamosi (Juni 24) kwenye Mkutano Mkuu wa klabu hiyo, amesema uzoefu wake wa kuzifundisha klabu kubwa na zenye mafanikio kama Wydad Casablanca ya Morocco, Esperance ya Tunisia na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, atauhamishia Jangwani na kuifanya timu hiyo kuwa tishio si ndani ya Tanzania tu, bali hata kwenye michezo ya kimataifa.

“Mambo Wananchi, mimi ni kocha kutoka Argentina, nimekuwa kocha zaidi ya miaka 20 barani Afrika, nimezifundisha klabu kubwa za Esperance, Mamelodi Sundowns na nimepata mafanikio mazuri nikiwa na timu hizo, nimefurahi sana kujiunga na klabu kubwa kama Young Africans na yenye historia nzuri katika soka la Tanzania na Afrika.

“Kwangu ni klabu kubwa yenye Mashabiki wengi wenye upendo, ninaamini kama tutaunganisha nguvu zetu pamoja Wanachama, Mashabiki, Viongozi na Benchi la Ufundi, Wachezaji na Wafanyakazi wengine, tutaendelea kupata mafanikio makubwa kuanzia pale tulipoishia,” amesema kocha huyo.

Amesema amefurahi kujiunga na klabu hiyo kubwa na kuwataka Wanachama na Mashabiki wa Young Africans kuwa na subira kwani atawasili nchini hivi karibuni.

Wasifu unaonyesha kuwa Kocha huyo mpya wa Young Africans analijua soka la Kiafrika kwani, historia yake inasema amezifundisha klabu nane za Afrika, tangu alipoanza kuzifundisha timu hizo mwaka 2000, zikiwamo pia CR Belouizdad na USM Alger za Algeria.

Historia ya kocha huyo inaonyesha kuwa ameifundisha timu moja tu ya nchini kwao Argentina ambayo ni Racing Club de Avellaneda mwaka 1998 hadi 1999 na ilikuwa ni mara ya kwanza kwenye wasifu wake wa ukocha.

Kocha huyo mwenye uzoefu wa miaka 23 kwenye ukocha wa timu mbalimbali barani Afrika, lakini nje ya bara hili pia amezifundisha klabu mbili za Falme za Kiarabu, ikiwamo Ittihad Kalba, Timu ya Taifa ya Burkina Faso akiwa kocha msaidizi, huku pia akizifundisha Al Ahly Tripoli ya Libya, Hassania Agadir ya nchini Morocco na Platinum Stars ya Afrika Kusini.

Achraf Hakimi kurudi Real Madrid
Wananchi: Waziri Mwigulu amekurupuka, hatushirikishwi