Wakati kikosi cha Young Africans kikiwa tayari kwa mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh, Kocha wa timu hiyo, Miguel Gamondi amesema mchezo wa kombe la AFCON kati ya Sudan na Jamhuri ya Kongo (DRC) uliochezwa Septemba 9 umemuongezea kitu katika kuwafahamu zaidi wachezaji wa wapinzani wao hao.

Miguel aliuangalia mchezo huo na kuwafuatilia wachezaji nane wa timu hiyo waliotoka kwenye kikosi cha Al Merrikh watakaocheza nao leo Jumamosi (Septemba 16).

Kwenye kikosi hicho cha Sudan, kilikuwa na wachezaji nane wa kikosi cha kwanza cha Al Merrikh na kocha Gamondi amewafuatilia wachezaji hao.

Gamondi, amesema amewaona nyota hao na tayari amewapa maelekezo wachezaji wake namna ya kukabiliana nao baadae leo Jumamosi (Septamba 16).

“Niliutazama ule mchezo baada ya kujua ina wachezaji wa Al Merrikh, wapo wachezaji nane na nimewaangalia kwa wale waliopata nafasi ya kucheza. hii imeniongezea mbinu namna ya kukabiliana nao na nimetoa maelekezo kwa wachezaji wangu namna ya kucheza nao, ni wachezaji wazuri,” amesema Gamondi.

Mastaa wa Al Merrikh waliocheza kwenye mchezo wa Sudan na DRC ni Mohamed Mustafa, Ramadan Agab, Bakhit Khamis na beki wa kati Mohamed Karshoum aliyecheza sambamba na beki wa Al Hilal, Mohamed Ahmed.

Wengine ni Ahmed Mahmoud na Mohamed Shambaly ambaye alitokea benchi na kati ya mastaa hao wenye uhakika wa kuanza kwenye kikosi cha kwanza kwenye mchezo wa leo Jumamosi (Septemba 16) dhidi ya Young Africans ni golikipa Mustapha, kiungo Agab, beki wa kati Kashroum na mshambuliaji Shambaly.

“Nilikuwa naangalia namna wanavyocheza na ubora wao, nilishawaona kwenye baadhi ya video za klabu yao, kama benchi la ufundi kwa kiasi kikubwa kazi yetu tumeifanya, kazi imebaki kwa wachezaji wetu ambao nina imani nao sana kutupa matokeo mazuri,” amesema Gamondi.

Amesema Al Merrikh ni timu kubwa na ina wachezaji wazuri ambao itawafanya wao (Young Africans) kucheza kwa tahadhari kwenye mchezo huo wa Ugenini.

“Ni jambo zuri sana kama timu kuona tutakuwa na mashabiki wetu wa kutosha uwanjani, hii itatupa hamasa sana, kwa kweli wachezaji wanajivunia kuwa na mashabiki wa aina hii,” amesema Gamondi.

Miezi sita: Lokassa ya Mbongou bado hajazikwa
Dkt. Mwinyi aelezea umuhimu wa Sayansi kwa nchi zinazoendelea