Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Miguel Angel Gamondi amesema ana kazi kubwa kuhakikisha washambuliaji wake wanatumia vyema nafasi za kufunga dhidi ya Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly Jumamosi (Desemba 02).
Young Africans itacheza mchezo huo nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kupoteza mchezo wa kwanza wa Kundi D ugenini dhidi ya CR Belouizdad kwa mabao 3-0.
Kocha huyo kutoka nchini Argentina amesema anaendelea kukiandaa kikosi chake vizuri lakini mabeki wake nao wana mkakati wao ili kuizuia safu ya ushambuliaji wa Al Ahly.
“Mchezo uliopita umekuwa darasa hatutaki kurudia tena makosa tunahitaji kutumia vyema uwanja wetu wa nyunmbani kwa lengo la kuhakikisha tunarudi kwenye ushindani japo haitakuwa rahisi kwani hatua tuliyopo inahitaji Pointi kwa kila timu kujihakikishia nafasi ya kusonga.”
“Benchi la ufundi, wachezaji na mashabiki wetu wanatambua ugumu wa huo mchezo tunaendelea kujiweka imara ili kuhakikisha tunasawazisha makosa tuliyoyafanya mchezo uliopita na kujihakikishia nafasi ya kusonga hatua inayofuata.” amesema Gamondi.
“Kuna kazi kubwa inahitajika kufanyika kwa wachezaji wangu ili tuweze kupata matokeo nyumbani naamini hilo litafanikiwa kutokana na maelekezo ya kiufundi niliyo wapatia;
“Malengo yetu ni kusonga hatua inayofuata na hilo naamini litawezekana kama wachezaji wangu watacheza kwa malengo na ushindani, kukosa matokeo kwenye mchezo wa kwanza haiwezi kuwa sababu ya kutukatisha tamnaa bado tuna nafasi ya kufanya vizuri hasa tukianza na matokeo mazuri nyumbani,” amesema
Young Africans ambayo imepangwa Kundi D na timu za CR Belouizdad, AI Ahly ya Misri na Medeama ya Ghana, itashuka Desemba 2, mwaka huu ikiwa kwenye uwanja wake wa nyumbani Benjamin Mkapa.