Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans wamesema wamefanya maandalizi ya kutosha kuelekea mechi yao dhidi ya Al-Merreikh ya Sudan Uwanja wa Azam Complex leo Jumamosi (Septemba 30) na kuweka wazi dhamira yao ya kutinga hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 25.
Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi ameeleza kuwa licha ya kufahamu kuwa klabu hiyo ina kiu ya kufika makundi, lakini yeye binafsi anahitaji kulifanikisha hilo kwa kuwa ni miongoni mwa yaliyomleta kuinoa timu hiyo.
“Tuna dakika 90 za kupambania tunachotaka kukipata, kufuzu makundi. Maandalizi yalikuwa mazuri na tulipata muda mwingi wa kujiandaa, tumefanya maandalizi makubwa kuhakikisha leo tunacheza mechi nzuri na kuwapa furaha familia ya wananchi.
“Kila kitu kipo sawa na nitaweka kikosi cha kwanza ambacho kitakuwa na mbinu tofauti na kwenye mechi ya ugenini, tutarekebisha makosa ya mechi ya kwanza ili tupate ushindi maana tutaingia uwanjani kama vile matokeo ni 0-0,” amesema Gamondi.
Young Africans ilipata ushindi wa mabao 2-0 kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Uwanja wa Pele, Kigali, na kwenye mechi ya leo Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 1.00 jioni, Young Africans inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote kuingia hatua ya makundi.
Kocha wa Al-Merreikh, Osama Nabieh amesema: “Japokuwa Young Africans ni timu ngumu kwa sasa lakini hapa kutafuta mnatokeo tumekuja na lolote linawezekana kama wao walipotufunga mechi ya kwanza.
“Dakika 90 za leo zitajibu maswali yote, sio kitu rahisi kufunga bao kwenye soka, tuliruhusu mabao mawili sababu tulifanya makosa ambayo kwenye soka yapo na tutayatumia pia makosa ya Yanga kwa ajili ya kufanikisha malengo yetu.”