Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi ameanza kumuandaa mbadala wa beki wa kushoto wa timu hiyo, Joyce Lomalisa ambaye atakosekana katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Medeama ya nchini Ghana.
Lomalisa atakosekana katika mchezo huo, kutokana na majeraha aliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Al Ahly ya nchini Misri ambao ulipigwa Jumamosi (Desemba 02), kwenye Uwanja wa Mkapa, jijini Dar es salaam.
Young Africans inatarajiwa kuvaana dhidi ya Medeama SC keshokutwa Ijumaa (Desemba 08) saa nne kamili usiku huko Ghana, kabla ya kurudiana kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam.
Gamondi amesema kuwa, hana hofu ya kukosekana Lomalisa, licha ya umuhimu alionao katika kikosi chake, kutokana na uwepo wa mbadala wake.
Gamondi amesema baada ya kupata ripoti ya madaktari ya kumkosa Lomalisa, haraka alianza kuwaandaa mabeki wawili wenye uwezo wa kucheza nafasi hiyo, ambao ni Nickson Kibabe na Kibwana Shomari.
Ameongeza kuwa anaamini viwango vya mabeki hao wote, na mmoja ndiye atakayechukua nafasi yake katika mchezo huo dhidi ya Medeama ambao, Young Africans wanahitaji ushindi ili wajiwekee nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya Robo Fainali.
“Nimejitahidi kutengeneza timu ambayo haimtegemei mchezaji mmoja katika kikosi changu, hivyo basi akikosekana mchezaji mmoja, baasi anakuwepo mwingine mwenye kiwango bora atakayeziba naafasi yake.
“Mchezo ujao dhidi ya Medeama, tutamkosa Lomalisa kutokaana na majeraha aliyoyapata katika mchezo uliopita dhidi ya Al Ahly, ambaye alishindwa kuendelea na mchezo huo katika kipindi cha pili.
“Baada ya kupata taarifa kutoka kwa madaktari za kumkosa Lomalisa katika mnchezo ujao dhidi ya Medeama, haraka nikaaanza kuwaandaa wachezaji wangu wawili watakaochukua nafasi yake ambao ni Kibabage na Kibwana.
“Ninaendelea kuwandaaa zaidi katika kambi yetu tutakayoiweka huko Ghana, kwa kuwapa mbinu za kuzuia na kuanzisha mashambulizi golini kwa mpinzani wetu, kwani mechi ambayo tunahitaji ushindi pekee,” amesema Gamondi.