Kocha Mkuu wa Young Africans Miguel Gamondi, amesema wachezaji wake wote ikiwa ni pamoja na Maxi Nzengeli, Aziz Ki na Jonas Mkude, ni lazima waongeze mashambulizi katika kila mchezo badala ya kujilinda.

Kocha huyo amebainisha kuwa, anafurahishwa na soka la kushambulia kwenda mbele kuliko kujipanga kuanzia kwenye lango lao jambo linalowapa nguvu wapinzani kuwalazimisha wachezaji wake wafanye makosa.

Gamondi amesema kuwa ili kupata ushindi kwenye mechi ni lazima kupeleka mashambulizi kwa wapinzani muda mrefu jambo litakalowapa nafasi ya kutengeneza makosa kwa wapinzani wao.

“Ikiwa tunacheza na wapinzani wetu ni muhimu kushambulia kwenda kwenye lango lao. Mtindo wa kurudisha pasi nyuma mara kwa mara huu unaruhusu makosa eneo letu jambo ambalo litasababisha tufungwe.

“Mpira ni mchezo wa makosa, ikiwa utafanya kosa ukiwa kwenye eneo lako nafasi ya kufungwa inakuwa karibu, hivyo ili kupunguza kasi hiyo ni muhimu kushambulia kwenda mbele muda wote kuwafuata wapinzani wetu,” amesema Gamondi.

Miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wakipenda kupiga pasi kuelekea langoni mwao ni pamoja na Mkude, Nzengeli na Aziz Ki.

Ikumbukwe kuwa, Young Africans msimu huu imecheza mechi mbili za Ligi Kuu Bara na kushinda zote, imefunga mabao kumi na haijaruhusu wavu wake kutikiswa, imekusanya pointi sita na kuongoza msimamo wa ligi hiyo.

Tumieni vikundi kutanzua uhalifu katika jamii- SSP Kahando
Viongozi wa Afrika wahimizwa kuwa na kauli moja