Kocha Mkuu wa Young Africans, Miguel Gamondi raia Argentina, ameanza kufungua faili lake la silaha kali kuelekea mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Mzunguuko wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Merrikh ya Sudan kwa kuwafanyisha mazoezi wachezaji wake mara mbili kwa siku.
Muargentina huyo amechukua uamuzi wa kuianza program hiyo kuelekea kuivaa Al Merrikh, mchezo wa kwanza ukitarajiwa kupigwa Rwanda, Septemba 16, mwaka huu, kabla ya mchezo wa marudiano Septemba 30, mwaka huu jijini Dar.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Young Africans, zinaeleza kuwa, benchi la ufundi la timu hiyo chini ya kocha huyo limefanya tathmini kubwa kuelekea mchezo huo baada ya kuwasoma wapinzani wao kupitia mikanda ya video waliyoinasa, hali iliyopelekea kubadilisha program zake kwa lengo la kuwaongezea utimamu wa kutosha wachezaji wake kabla ya mchezo huo.
“Unajua mwalimu alitoa mapumziko mwishoni mwa juma lililopita ndiyo maana Jumatatu (Septemba 04) tulianzia ufukweni kwa ajili ya wachezaji kurudisha utimamu wao kabla ya kurejea uwanjani kuendelea na ratiba zengine za kiufundi, lakini baada ya kuwaangalia wapinzani ameona kuongeza maarifa ya kimbinu kwa wachezaji kupata muda wa kufanya mazoezi mara nyingi.
“Unajua mwalimu mwenyewe na benchi lake ndiyo wanajua wanachokitaka baada ya kuangalia wapinzani ndiyo maana wamebadilisha program kwa kuongeza muda zaidi wa kufanya mazoezi kulingana na ukubwa wa mchezo ambao upo mbele yetu kwa sasa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Kwa upande wa Gamondi, alisema: “Mkakati wangu mkubwa Pamoja na benchi la ufundi ni kuangalia jinsi gani tunapata matokeo mazuri kwa kuhakikisha tunaenda hatua ya makundi hali ambayo inatufanya tuchukue muda mwingi kwenye uwanja wa mazoezi japo kuwa baadhi ya wachezaji hatupo nao ila naamini tutakuwa sawa kabla ya mchezo wenyewe.”