Baada ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans kukata tiketi ya kucheza hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuwang’oa Al Merrikh ya Sudan kwa jumla ya mabao 3-0, Kocha Miguel Gamondi amethibitisha kwamba bado kikosi chake kina uhitaji.
Gamondi amesema baada ya kikosi chake kufuzu bado anahitaji maboresho zaidi ya kuongeza watu bora kwenye timu hiyo.
Gamondi amefafanua akisema hatua ambayo Young Africans imeingia haitakuwa rahisi ambapo anataka kukiongezea nguvu zaidi kikosi chake kupitia dirisha lijalo la usajili.
“Kufuzu ni hatua moja lakini lazima tufanye tathimini ya kina juu ya kikosi chetu tutakwenda kukabiliana na timu kubwa na ngumu zaidi ambazo zimefuzu kama sisi,” amesema Gamondi.
“Tutaangalia ni namna gani na maeneo gani tutakayoyaboresha baada ya vikao na viongozi wangu wa klabu wakati tunasubiri kujua ni timu zipi tutapangiwa nazo.”
Hata hivyo, Gamondi amesema hatua hiyo itategemea na bajeti ya klabu lakini pia kufanya hesabu sahihi ya wachezaji gani wa kupunguza kwa vile tayari Young Africans ilishakamilisha idadi ya wachezaji wa kigeni kikanuni.
“Kusajili kuna mambo mengi ya kuzingatia ni lazima kwanza tukutane na viongozi. Kuna bajeti inahitajika lakini pia tayari hapa kwetu tuna wachezaji kumi na mbili utaona kwamba lazima Kuna mchakato upite,” amesema
Ingawa Gamondi hakutaka kuonyesha moja kwa moja lakini taarifa za ndani ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba kocha huyo bado anasisitiza kuletewa mshambuliaji wa kati mwenye makali ya kujua kufunga.