Kocha Mkuu mpya wa Young Africans, Miguel Gamondi anatarajiwa kuwasili jijini Dar es salaam kwa ajili ya kukamilisha taratibu za kusaini mkataba na kuweka sawa mazingira ya kibarua chake kipya akiwa na miamba hiyo ya Tanzania Bara.

Kocha huyo raia wa Argentina ametua Young Africans akichukua mikoba ya Nasreddine Nabi ambaye ameachana na timu hiyo mwishoni mwa msimu uliopita na kuomba kutosaini mkataba mpya akitaka kwenda kusaka changamoto sehemu nyingine.

Meneja wa Habari wa Young Africans, Ally Kamwe amesema mbali na kukamilisha taratibu za mikataba lakini ujio wa kocha huyo pia utachangia katika kuchagua makocha wasaidizi pamoja na mchakato wa maboresho ya kikosi chao cha msimu ujao.

“Gamondi anakuja kupendekeza watu watakaomsaidia kwa maana kocha msaidizi, kocha wa viungo na kocha wa makipa, lakini pia tutampa ripoti iliyoachwa na mtangulizi wake Nabi na yeye atatupa mapendekezo yake kwamba ni wachezaji gani angependa tumwongeze,” amesema Kamwe.

Meneja huyo amesema baada ya hapo kikosi chao kitaanza maandalizi ya msimu ujao wakiwa kwenye kambi yao ya siku zote Avic Town, Kigamboni kujiandaa na wiki ya Mwananchi pamoja na mashindano maalumu ya Ngao ya Jamii ambayo msimu ujao itashirikisha timu nne zilizo nafasi nne za juu kwenye ligi.

Kamwe amesema mpaka sasa mchakato wa usajili unakwenda vizuri kwa kufuata maelekezo ya ripoti iliyoachwa na Nabi pamoja na maelekezo kutoka kwa Gamondi ambaye ndiye atakayesimamia zaidi suala hilo la kupendekeza wachezaji anaowahitaji.

Kwa mujibu wa Kamwe, Young Africans inatarajia kusajili wachezaji sita wapya ambapo kati yao watatu watakuwa raia wa kigeni na waliobaki ni wazawa.

Pep Guardiola akutana na Declan Rice
Tottenham Hotspur: Kane hauzwi kwa bei yoyote