Mshambuliaji Gareth Bale ameungana na wachezaji wa kikosi cha kwanza cha Real Madrid katika mazoezi ya kuelekea mchezo wa hatua ya 16 bora wa michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya SSC Napoli.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 27, alikua nje ya uwanja tangu mwezi Novemba mwaka jana, alithibitisha kurejea kwake mazoezini kwa kuweka picha na taarifa kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter.
Kurejea kwa Bale, ni faraja kwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Wales Chris Coleman, ambaye atakua na kazi ya kuhakikisha kikosi chake kinachomoza na ushindi kwenye mchezo wa kuwania kufuzu fainali za kombe la dunia dhidi ya jamuhuri ya Ireland utakaochezwa mjini Dublin mwezi ujao.
Wales inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa kundi D, ikiwa na point nne nyuma ya jamuhuri ya Ireland inayoongoza kundi hilo kufuatia ushindi walioupata kkwenye michezo mitatu.
Meneja wa Real Madrid Zinedine Zidane alithibitisha kurejea kwa Bale alipozungumza na waandishi wa habari siku ya ijumaa, na anatarajia kumtumia katika mchezo dhidi ya SSC Napoli.
Hata hivyo pamoja na kukosekena kwa mshambuliaji huyo tangu mwezi Novemba mwaka jana, bado kikosi cha Real Madrid kilionyesha kupambana vilivyo na kuendelea kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi ya nchini Hispania (La Liga).
Siku ya jumamosi Real Madrid walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao matatu kwa moja dhidi ya Osasuna, hatua mbayo iliiwezesha klabu hiyo kuendelea kukaa kileleni kwa tofauti ya point moja dhidi ya FC Barcelona, huku ikiwa na mchezo mmoja mkononi dhidi ya Celta Vigo.