Kocha wa timu ya taifa ya England, Gareth Southgate amemmwagia sifa kinda wake Jude Bellingham, kufuatia kuonyesha kiwango bora na kuisaidia timu kupata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Italia katika mchezo wa kufuzu michuano ya Euro 2024.
Kinda huyo mwenye umri wa miaka 20, alionyesha kiwango bora katika mchezo huo kwa kusababisha mkwaju wa Penati na kutoa pasi moja ya mwisho, mechi iliyochezwa juzi Jumanne (Oktoba 17) Uwanja wa Wembley, London England.
Katika mchezo huo, Mshambuliaji Harry Kane alifunga bao la kwanza dakika ya 32 kwa mkwaju wa Penati, Marcus Rashford akifunga la pili dakika ya 57, kabla ya Kane kufunga bao la tatu dakika ya 77, huku bao pekee la Italia likiwekwa kimiani na Gianluca ScamaCca katika dakika ya 15.
Kocha Southgate amesema Bellingham alionyesha kiwango kizuri na kwamba anaamini atakuja kuwa mmoja wa wachezaji bora Duniani.
Tumecheza na moja ya taifa kubwa na kila mchezaji alitimiza majukumu yake vizuri kuhakikisha tunafikia malengo.
“Ulikuwa mchezo mgumu wenye upinzani mkali ninampongeza Bellingham kwa kuonyesha kiwango bora, ninaamini atakuja kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi Duniani.
“Ana umri mdogo, lakini ameonyesha ukomavu wa hali ya juu na ninafurahia kuwa na mchezaji kama Bellingham,” amesema Kocha Southgate.
England tayari imeshafuzu michuano ya Euro 2024 huku ikibakisha mechi mbili mkononi dhidi ya Malta na baadae kuifuata Macedonia Kaskazini mwezi ujao.