Gari la Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema limechomoka matairi likiwa barabarani ambapo imedaiwa kuwa lilifunguliwa nati na ‘watu wasiojulikana’.

Lema amesema kuwa yeye na mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari walikuwa wamepanga kusafiri na gari hilo kuelekea jijini Dar es Salaam kuwasilisha ushahidi wao wa tuhuma za rushwa kwenye Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Amesema alishtukia kuwa gari lake haliko salama aliposikia mlio kwenye matairi baada ya kuliendesha umbali mdogo, ndipo alipoamua kulipaki kwenye hoteli ya ‘Equator’.

Mbunge huyo ameeleza kuwa kutokana na kulitilia mashaka aliamua kuliacha na kuomba lifti kwenye gari la Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Isack Joseph kuendelea na safari ya kwenda Dar es Salaam.

“Leo asubuhi nikamtuma dereva wangu akachukue gari pale kwenye hoteli ya Equator ili alipeleke gereji lakini baada ya hatua chache lilichomoka matairi,” Mwananchi inamkariri Lema.

Ameeleza kuwa anaamini ‘watu wasiojulikana’ ndio waliofungua nati kwenye gari hilo likiwa nyumbani kwake, hivyo ameagiza kampuni ya ulinzi inayofanya kazi kwake kufanya uchunguzi na kupitia kamera za CCTV kuwabaini waliohusika.

Aidha, amesema amemuagiza dereva wake atoe taarifa katika kituo cha polisi kwenye eneo hilo.

Airtel yazindua ofa ikisherehekea wiki ya huduma kwa wateja
Jafo awapongeza wananchi Kisarawe