Aliyekua beki wa pembeni na nahodha wa klabu ya Manchester United, Gary Neville ameutaka uongozi wa klabu hiyo kutochukua maamuzi ya haraka dhidi ya meneja Jose Mourinho na badala yake ameshauri kumpa muda mkuu huyo wa benchi la ufundi.
Neville ametoa ushauri huo kwa kuhofia huenda uongozi wa Man Utd ukachukua maamuzi ya kumtimua Mourinho, baada ya kuanza vibaya mshike mshike wa ligi kuu ya soka nchini England kwa kupoteza michezo miwili, huku akishinda mmoja pekee.
Msukumo wa kupoteza kazi kwa Mourinho, uliongezeka usiku wa kuamkia leo kufuatia kikosi chake kukubali kufungwa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Tottenham Hotspur, na kuifanya klabu hiyo kuporomoka hadi katika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi huku ikijiandaa kuwa mgeni wa Burnley mwishoni mwa juma hili.
“Tuliona Louis van Gaal alitimuliwa akiwa ameshinda ubingwa wa kombe la FA, tukaona David Moyes alifukuzwa kazi michezo minne ya ligi ikisalia kabla ya msimu kufikia kikomo, jambo hili sio salama kwa klabu endapo tutaendelea na mfumo wa kuwafuta kazi mameneja ambao wanahitaji kupewa muda,” alisema Neville alipohojiwa kwenye kipindi cha Monday Night Football, kilichorushwa na televisheni ya Sky Sports.
“Ninakubaliana na kila mmoja anaepingana na kinachoendelea kwa sasa, lakini siungi mkono taratibu ambazo zinafikiriwa kuchukuliwa kwa Mourinho zaidi ya kutaka abaki ili kuendelea kuijenga Man utd inayohitaji kufikia lengo la kutwaa mataji miaka michache ijayo,” aliongeza.
Alisisitiza kuwa hakuna timu itakayoweza kupata mafanikio kwa kumfukuza kila kocha, kila kukicha! na kwamba wanahitaji muda kufanikisha wanachokihitaji.
Mourinho alisaini mkataba mpya mwezi Januari mwaka huu ambao utafikia kikomo mwaka 2020, na kama atafukuzwa klabuni hapo, Man Utd italazimika kumlipa fidia ya mamilioni ya Pauni.