Nahodha na Beki wa zamani wa Man Utd Gary Neville amemsifu Declan Rice, huku kiungo huyo wa Arsenal akifunga bao lake la kwanza kwa klabu hiyo katika ushindi wa mabao 3-1 walioupata Washika Bunduki hao dhidi ya Mashetani Wekundu, Jumapili (Septemba 03).
Ilionekana kuwa wapinzani hao wawili wa zamani walikuwa wakielekea kugawana pointi wakati mchezo ulipoingia dakika nane za nyongeza wakiwa wamefungana bao 1-1 kwenye mchezo wa Ligi Kuu England.
Lakini Rice alipata nafasi upande wa kushoto wa kisanduku kutoka kona ya Arsenal na kumfyatua Andre Onana kupitia kwa mpira uliomgonga Jonny Evans na kuwapa bao la pili vijana wa Mikel Arteta.
Akichambua mchezo kupitia Sky Sports, Neville alizungumzia bao la Rice na kudai ni wakati kama huu ndio uliowafanya Washika Bunduki hao kuvunja benki na kutoa kitita cha rekodi kwa ajili ya kiungo huyo wa kati wa England.
“Declan Rice amekuja katika klabu hii ya soka kuleta tofauti,” alisema Neville.
“Anawasalimu watu wanaomuamini mbele yake. Mashabiki wa Arsenal wanampenda, wamepata shujaa mpya na amecheza mechi chache tu.
“Ndio maana alikuja hapa, ndio maana walilipa fedha nyingi. Dakika kubwa, mechi kubwa.”
Rice alifanya mashabiki kulipuka kwa shangwe kwenye dimba la Emirates huku akizongwa na wachezaji wenzake na, kuwakimbilia mashabiki kushangilia bao la dakika za lala salama.
Furaha hiyo haikuishia hapo, kwani Gabriel Jesus aliongeza bao la tatu dakika ya 98 na kuipa Arsenal uhakika wa alama zote tatu.
Hapo awali, Marcus Rashford alikuwa ameiweka Man United uongozini na kuanza mchezo huo kwa kasi.
Lakini Arsenal walipata bao ndani ya dakika moja kupitia kwa Martin Odegaard na kusawazisha bao hilo.
Kikosi cha Erik ten Hag kilifikiri kuwa kimeshinda mchezo huo wakati Alejandro Garnacho alipokimbia na kuuweka mpira wavuni, lakini VAR ikalikataa bao hilo kwani ilionesha kuwa alikuwa ameotea.