Gwiji wa Soka nchini England Gary Neville amewataja wachezaji watatu wa Arsenal ambao wanapaswa kujipambanua wenyewe ili kuweka mambo sawa kwenye mbio za ubingwa msimu huu.
Arsenal iliangusha alama mbili muhimu usiku wa Ijumaa iliyopita baada ya kupata sare ya mabao 3-3 na timu ya chini kwenye msimamo, Southampton tena uwanjani kwao Emirates.
Kikosi hicho cha Mikel Arteta ni kama kimeandamwa na sare baada ya kupoteza alama mbili mbili pia kwenye michezo miwili iliyopita dhidi ya Liverpool na West Ham kabla ya Southampton iliyofanya kuwa sare ya tatu mfululizo.
Kwa sasa Arsenal inaongoza Manchester City kwa tofauti ya alama tano, lakini wapinzani wao hao kwenye mbio za ubingwa wenzao wana mechi mbili mkononi.
Na wakati Man City ikitarajia kuikaribisha Arsenal uwanjani Etihad keshokutwa Jumatano, mchezo ambao Arteta na chama lake anatapaswa kuepuka kipigo, Neville amesema: “Kuna wachezaji wazoefu wa Arsenal wan ahitaji kusimama mstari wa mbele. Katika mechi tatu zilizopita, wachezaji hao wenye uzoefu kama hawakuwapo. “Vijana wanahitaji kuwekwa sawa. Zinchenko, Gabriel Jesus, Thomas Partey wameshindwa kuonyesha ukomavu wao. Kuna hizi siku zilizobaki kabla ya mechi ijayo. Wanahitaji kujipambanua!”