Shirikisho la soka nchini TFF, limetuma salamu za shukrani kwa Gavana wa Jimbo la Akwa Ibom, Gabriel Emmanuel  kwa zawadi ya dola 10,000 za Marekani (sawa na Sh milioni 21.5) kwa timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania ‘Taifa Stars’ baada ya kuonesha mchezo mzuri na wa upinzani dhidi ya wenyeji Super Eagles ya Nigeria uliofanyika Uwanja wa Kimataifa wa Godswill Akpabo, mjini Uyo.

Taifa Stars ilicheza mechi hiyo Jumamosi Septemba 3, 2016 katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON 2017). Katika mchezo huo ambao mashabiki waliingia bure, Taifa Stars ilifungwa bao 1-0 mara baada ya kuibana Super Eagles hivyo kumsukuma Gavana huyo kuandaa hafla ya chakula cha jioni ambako mbali ya kuizawadia Stars, pia aliizawadia Super Eagles dola 35,000 za Marekani.

Taifa Stars ilitua Dar es Salaam usiku wa kuamkiia leo Septemba 5, 2016 ambako baadhi ya wachezaji walipelekwa  Hoteli ya Urban Rose, iliyoko katikati ya Jiji la Dar es Salaam wakati wengine hususani wale wa timu ya Azam FC walichukuliwa na viongozi wao kwa ajili ya safari ya kwenda Mbeya ambako Jumatano wanatarajiwa kucheza na Tanzania Prisons kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara utakaofanyika Uwanja wa Sokoine mjini humo.

Kadhalika wachezaji wa Young Africans nao walichukuliwa kwa ajili ya safari ya kwenda Mtwara ambako watakuwa na mchezoi dhidi ya Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini humo wakati nyota wa Simba watabaki hapa Dar es Salaam kwani Jumatano itakuwa na kibarua dhidi ya Ruvu Shooting kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom.

Wakati nyota 18 wakitua Dar es Salaam, Nahodha wa timu hiyo, Mbwana Samatta aliishia Nairobi, Kenya ambako aliunganisha ndege ya kwenda Brussels, Ubelgiji.

Licha ya mchezo huo kuwa sehemu ya mchuano wa kuwania nafasi ya kucheza fainali hizo za AFCON 2017 huko Gabon, lakini ulikuwa ni wa kukamilisha ratiba baada ya Misri kufuzu kwa fainali hizo kutoka kundi G ambalo mbali ya Nigeria na Tanzania, pia ilikuwako Chad ambayo iliyojitoa katikati ya mashindano.

Semina Elekezi Soka La Wanawake Yapigwa Kalenda
Mbeya City Yawasili Nyumbani, Kuvaana Na Azam FC J.Mosi