Kiungo wa kati wa FC Barcelona, Pablo Martín Páez Gavira ‘Gavi’ anatarajiwa kuwa nje ya uwanja kwa muda wa miezi nane hadi kumi baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti mwanzoni mwa juma hili.
Gavi mwenye umri wa miaka 19, aliumia goti wakati akiichezea Hispania dhidi ya Georgia katika mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Ulaya ‘Euro 2024’.
Kiungo hatakuwa sehemu ya kikosi cha FC Barcelona katika kipindi cha msimu huu kilichosalia, na pia atazikosa Fainali za Euro 2024 akiwa na Hispania, zinazotarajiwa kuanza kuanza Juni 14, mwakani nchini Ujerumani.
“Gavi amefanyiwa operesheni iliyofaulu kwenye goti lake la kulia lililochanika pamoja na mshono,” taarifa ya Barca ilisema juzi.
“Alisimamiwa na daktari wa klabu, Joan Carles Monllau wakati wa upasuaji huo katika Hospitali ya Barcelona.”
Kocha wa Barca, Xavi Hernández, alisema wiki iliyopita Gavi, ambaye alishinda tuzo ya mchezaji bora kijana wa Ulaya Golden Boy’ mwaka 2022, hawezi kubadilishwa kwa sababu ya “moyo, shauku na ujasiri.”
Gavi amekuwa mchezaji wa muhimu wa Barca na Hispania msimu huu, alikosa mechi mbili pekee, zote kwa klabu yake kutokana na kusimamishwa.
Wakati wa jeraha lake, ni Marc André ter Stegen na lIkay Gündogan pekee waliokuwa wameichezea Blaugrana dakika nyingi zaidi.
Kwa jumla, ameichezea Barca mechi 111 na tangu alipoanza kucheza mechi yake ya kwanza akiwa na umri wa miaka 17 mnamo Agosti, 2021, hakuna mchezaji ambaye ameichezea klabu hiyo michezo zaidi.
Ukali wa jeraha lake umesikika kote Hispania, na chanzo kililambia ESPN Rais wa Real Madrid, Florentino Pérez, alikuwa miongoni mwa watu waliomtumia kiungo huyo ujumbe wa kumtakia heri.
Barca ilirejea uwanjani bila Gavi na kutoka sare ya 1-1 na Rayo Vallecano mwishoni mwa juma lililopita (Jumamosi) na kumenyana huku juzi iliifunga FC Porto mabao 2-1 katika Ligi ya Mabingwa ya UEFA na kufuzu hatua ya 16 bora kwa mara ya kwanza tangu 2021.
Xavi ametiwa nguvu na kurejea kwa viungo Pedri na Frenkie de Jong katika wiki za hivi karibuni, huku nahodha, Sergi Roberto pia akiwa fiti.