Gazeti la New York Times limeshutumiwa vikali kwa kuchapisha picha za miili ya watu waliopoteza maisha katika shambulio la hoteli ya kifahari ya DusitD2 jijini Nairobi.
Gazeti hilo lenye makao yake makuu nchini Marekani limechapisha picha za marehemu wakionekana dhahiri kuwa na matundu ya risasi kwenye miili yao na kulowa damu.
Wakenya walimimina hasira na kukirihishwa kwao kwa hatua hiyo ya New York Times kwa kuandika ujumbe katika mitandao ya kijamii ikwemo Twitter.
Baadhi hata walilinganisha namna walivyoripoti matukio ya uhalifu nchini Marekani tofuati na walivyofanya kwa mkasa huu Kenya.
Aidha jana majira ya saa 9 alasiri jijini Nairobi kulitokea shambulio la risasi katika hoteli ya kifahari mtaa wa Riverside lililofanywa na kundi la kigaidi la Al-shabab ambao walikiri kufanya shambulio hilo lililosababisha vifo vya watu 14.
Hata hivyo mapema ya leo Rais Uhuru Kenyatta alitangaza kuawa kwa magaidi wote waliofanya tukio hilo la kigaidi nchini humo.