Mchambuzi wa Michezo nchini Tanzania Geoffrey Lea ameshangazwa na Maamuzi ya Shirikisho la Soka ‘TFF’ kupitia kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, dhidi ya Kiungo kutoka visiwani Zanzibar Feisal Salum ‘Fei Toto’.
Feisal aliomba kurejewa kwa maamuzi ya shauri lake dhidi ya Young Africans, lakini bado Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ikaendelea kusimamia msimamo wake wa kumtambua kama Mchezaji halali wa Klabu hiyo ya Jangwani.
Geoffrey amesema sakata la kiungo huyo linamshangaza kwa sababu ni wazi Mikataba ya Wachezaji inapaswa kuwa na kipengele cha kuvunjwa, lakini imekuwa tofauti kwa Feisal.
“Mikataba yote ya Wachezaji Duniani ni lazima iwe na kipengele cha kuvunja mkataba muda wowote hata kama alisajiliwa jana.”
“Feisal Saum kama alikosea kuvunja mkataba TFF walitakiwa wamuadhibu Feisal kwa kulipa faini au kufungiwa.”
“Unatuambia kuwa shauri tumetupilia na Feisal ni mchezaji wa Yanga kwa maana Yanga wana mikataba yao ambayo haihusiani na FIFA kwamba haiwezi kuvunjwa.”
“Kuna ushamba mwingi kwenye hili sakata ila TFF itoe nakala ya hukumu hii kesi ni nyepesi kwa Feisal kama itaenda CAS.” amesema Geoffrey