Uongozi wa Klabu ya Geita Gold FC unaendelea kuwa kwenye Mchakato wa kukiboresha kikosi chao, kupitia Dirisha Dogo la Usajili ambalo rasmi litafunguliwa Desemba 15.
Geita Gold FC tayari imeshathibitisha kummasa Mshambuliaji Ditram Nchimbi ambaye atakua huru Desemba 15, kufuatia mkataba wake na klabu ya Young Africans kuelekea ukingoni.
Taarifa nyingine zinazoihusu klabu hiyo upande wa usajili ni harakati za kuwanyemelea wachezaji wengine wa Young Africans, ambao mikataba yao ipo ukingoni katika kipindi hiki.
Miongoni mwa wachezaji wanaotajwa kuwaniwa na Geita Gold FC ni Kiungo Mkabaji kutoka DR Congo Mukoko Tonombe, ambaye hatma yake ndani ya kikosi cha Wananchi bado haijafahamika.
Mmoja wa viongozi wa Gaita Gold FC ambaye hakutaka jina lake kuanikwa hadharani amesema, wanaendelea na mchakato wa mazungumzo ya kuangalia uwezekano wa kumsajili Kiungo huyo, ambaye Msimu uliopita alitikisa katika Mshike Mshike wa Ligi Kuu.
“Tunaendelea kuzungumza naye na wengine wanaomaliza mikataba yao, tukikamilisha tutaweka wazi.”
“Ni vigumu kusema lini mazungumzo yatakamilika, maana mazungumzo yanaweza kuchukuwa muda fulani, lakini asilimia kubwa tumeshaafikiana mambo ya msingi.” amesema kiongozi huyo
Wachezaji wengine wa Young Africans ambao huenda wakaondoka wakati wa Dirisha Dogo la Usajili ni Mukoko Tonombe, Adeyun Saleh na Yassin Mustapha na Shaibu Ninja ambaye ananyemelewa na Namungo.